Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA
Asisitiza Watanzania kuwa sehemu ya Mkakati
Aeleza athari za matumizi ya Nishati isiyo safi
Atoa hofu ya Gesi kulipuka
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mhe. Zainabu Katimba ametoa rai kwa wananchi kuunga mkono kwa vitendo Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ambayo ni Ajenda iliyoanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Nyakati zimebadilika, tuunge mkono juhudi za Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kutumia nishati safi kama gesi, umeme na nyinginezo. ” Amesema Mhe. Katimba
Ameongeza kuwa, watanzania wanapaswa kuwa sehemu ya Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia na kuonesha mabadiliko kwa vitendo kwa kutoka kwenye matumizi ya nishati zisizo safi na salama.
Aidha, amesisitiza kuwa, matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia yatapunguza kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira ambapo takwimu zinaonesha kila mwaka takribani hekta 469,000 za msitu zinateketea kwa sababu ya shughuli mbalimbali za kibinadamu ikiwemo matumizi ya nishati zisizo safi za kupikia (kuni na mkaa).
“Tukitumia Nishati Safi ya Kupikia hatutaokoa mazingira peke yake bali afya za watu pia kwani takribani watu 33,000 hupoteza maisha kwa sababu ya matumizi ya nishati zisizo safi, hii ni kutokana na mazingira ya jikoni ya moshi, hewa nzito ambayo huleta athari katika mfumo wa upumuaji.” Ameongeza Mhe. Katimba
Kuhusu mtazamo wa kuwa gesi inayotumika majumbani kupikia inalipuka, Mhe. Katimba amesema kuwa gesi hiyo ni salama kwa matumizi husika.