11 views 2 mins 0 comments

RAS TABORA:MKOA WA TABORA TUMEPIGA VITA MAFUNDI UMEME VISHOKA

In BIASHARA
September 18, 2024

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

Meneja wa EWURA Kanda ya Magharibi, Mha. Walter Christopher akizungumza na wadau wa sekta ndogo ya umeme wakiwamo mafundi, wakandarasi na wawakilishi wa taasisi mbalimbali wakati wa semina ya kuwajengea uwezo mafundi umeme wa mkoa wa Tabora leo 17 Septemba 2024
Katibu Tawala Mkoa wa Tabora, Dkt John Mboya, akizungumza na mafundi umeme wa mkoa na wadau wa sekta hiyo wakati wa semina iliyoandaliwa na EWURA kuwahimiza kutekeleza matakwa ya sheria na kanuni zinazosimamia sekta hiyo, mjini Tabora leo Septemba 17, 2024



Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dkt John Mboya, akifungua semina ya siku moja kwa mafundi umeme wa mkoa huo, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora,Paul Matiko Chacha, leo 17 Septemba 2024,amewasihi  mafundi umeme wote mkoani humo kuhakikisha wanakuwa na leseni za ufungaji mifumo ya umeme zinazotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kwa  mujibu wa Kifungu cha. 8 (h) cha Sheria ya Umeme,Sura  Na. 131.

“Kuanzia  leo, mkoa wa Tabora tumepiga vita mafundi vishoka, na ni  imani yangu kwamba baada ya semina hii kila asiye na leseni ataomba leseni ili afanye kazi kwa uhalali, ninawasihi sana tusipoteze fursa hii kwani mkoa wetu una miradi mingi ambayo ni fursa kwa mafundi umeme na kuanzia sasa vishoka wote hawatapewa kazi mpaka pale watakapokuwa na leseni ya EWURA,” alisema.



Meneja wa EWURA Kanda ya Magharibi, Mhandisi Walter Christopher, alisema semina hiyo iliyowashirikisha mafundi umeme na wadau zaidi ya 150, ililenga kuwajengea uwezo wataalam na wadau hao kuhusu sheria, kanuni, miongozo na utaratibu wa utendaji kwenye shughuli za ufungaji wa mifumo ya umeme.

Wadau wengine walioshiriki semina hiyo ni Wakala wa Usimamizi wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Shirika la Ugavi wa Umeme  nchini (TANESCO), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Wakala wa Majengo (TBA) na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA).

Mafundi umeme wanaweza kuomba leseni kupitia mfumo wa LOIS unaopatikana kwenye tovuti ya EWURA www.ewura. go.tz na kupakua fomu ya kukamilisha ufungaji mifumo ya umeme katika tovuti hiyo hiyo au kuwasiliana na EWURA kwa simu 0800110030, mitandao ya kijamii au   barua pepe; info@ewura.go.tz.

/ Published posts: 1212

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram