Na Madina Mohammed DAR ES SALAAM WAMACHINGA
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI anayeshughulikia Miundombinu, Mhandisi Rogatius Mativila amesema kuwa ili kufikia ujenzi wa kilomita 144,430 ya barabara ya ‘network’ ambayo iko chini ya TARURA wamekuwa wakihangaika na teknolojia mbalimbali ili angalau watumie fedha kidogo ziweze kujenga sehemu kubwa iwe inapitika.
Mativila ameyasema hayo leo Septemba 6, 2024 alipokuwa anazungumza na Waandishi wa Habari kwenye maonesho ya wiki ya Waandisi katika ukumbi wa Mlima City, Dar es Salaam ikiwa ni siku ya pili na ya mwisho tangu yalipofunguliwa Septemba 5, 2024.
“Ukiacha kwa kujenga madaraja kwa mawe ambapo tunapunguza gharama karibu asilimia 70, lakini pia tuna teknolojia ya kutumia ‘chemical’ kuboresha udongo uliyoko pale ukawa imara barabara zikaweza kudumu, hiyo yote ni Uhandisi na kama unayoona leo wamekuja hapa kwenye ‘Enginers Day’ wanaonesha nao wanafanya nini ambavyo ni vya ‘engineering’,” alisema.
Aidha Naibu Katibu Mkuu huyo TAMISEMI amesema kuwa teknolojia hizo zimewasaidia sana kupunguza gharama ili kuhakikisha hiyo ‘network’ inapitika ambayo ni kubwa sana na inagusa wananchi wengi waliyopo vijijini ambapo kuna uzalishaji mkubwa wa mazao.
“Kwa hiyo sehemu hizo zenye vikwazo zisizopitika kama za madaraja, ukijenga daraja hilo la bei ‘chip’ maana yake unaweza kujenga sehemu nyingi.
“Bilioni moja ambayo ungeweza kujenga daraja moja unajenga madaraja matatu ya mawe, lakini pia ukatumia udongo uliyopo kwa kutumia ‘chemical’ zilizopo za kisasa ili kuhakikisha badala ya kutafuta mbali udongo unapata palepale unakuwa umepunguza gharama, kwa fedha kidogo unakuwa umefanya kazi kubwa na ‘network’ kubwa kuwa inapitika”, alisema Mativila.