32 views 3 mins 0 comments

TUGHE YAMUUNGA MKONO RAIS SAMIA YAPELEKA WATALII 800 HIFADHI YA NGORONGORO

In KITAIFA
August 30, 2024

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

Wageni zaidi ya 800 kutoka Chama cha oWafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) wamefanya ziara ya kihistoria katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro jana tarehe 29 agosti, 2024.

Ziara hiyo ambayo imefanyika baada ya wajumbe wa TUGHE kumaliza semina iliyofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 26/08/2024  ina lengo la kuwaleta pamoja waajiri na wafanyakazi ili kupata uwelewa wa pamoja, kujadili na kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza mahala pa kazi.

Akiongoza ujumbe huo Mwenyekiti wa TUGHE Taifa Bw. Joel George Kaminyoge amesema lengo la ziara yao ni kutoa hamasa ya utalii wa ndani na kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kukuza utalii ambapo ziara hiyo imewapa fursa wanachama wao   kujionea vivutio vya kipekee vinavyopatikana hifadhi ya Ngorongoro.

“Leo tumekuja na wanachama zaidi ya 800 kutembelea Kreta ya Ngorongoro kujionea moja kati ya vivutio bora vya dunia ambavyo ni sehemu ya urithi wa dunia,  Tunaamini kwamba ziara yetu italeta tija na hamasa kwa wakuu wa taasisi kuwa na utaratibu wa kuwapeleka watumishi wao kufanya utalii wa ndani katika vivutio mbalimbali nchini” Alisema Bw. Kaminyoge

Akiwapokea wageni hao, Meneja wa huduma za Utalii na masoko wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Bi.Mariam Kobelo, alisema kwamba Mamlaka hiyo ipo tayari kuendelea kupokea makundi mbalimbali ya  wageni na kuwahakikishia kuwa wanapata huduma bora ili kuendelea kutqngaza hifadhi hiyo  na kuimarisha utalii ndani.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tanzanite Cooperates L.t.d aliyeratibu ziara hiyo Bi. Elina Mwangomo, ameleza kuwa kwa sasa kuna ongezeko kubwa la watalii wa ndani hali inayoongeza hamasa kwa wadau wa utalii kuendelea kuboresha huduma zao huku akieleza kuwa Ngorongoro imekuwa moja kati ya eneo ambalo linapendwa zaidi na wageni na watalii kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.

Bi. Jackline Ngoda ambaye ni mmoja kati ya wanachama waliotembelea Hifadhi hiyo ameonesha kufurahishwa  na ziara hiyo baada ya kujionea Wanyama mbalimbali ikiwepo wanyama wakubwa watano (Big 5) wakiwa katika maeneo yao ya asili.

“Kwa ujumla tumeona Wanyama mbalimbali, wakiwemo Simba, Nyati, Tembo, Swala, nyumbu, viboko, pundamilia na wengine wengi, tumeweza kuona uzuri wa kipekee wa Kreta ya Ngorongoro na napenda kuwaambia watanzania wenzangu waje kutembelea Ngorongoro na kujionea uzuri wake wa asili. Alisema Jackline.

Ziara hii ni sehemu ya juhudi za TUGHE kuwaleta pamoja waajiri na wafanyakazi wa taasisi za Serikali kupata nafasi ya kujifunza na kujenga uhusiano mzuri na ushirikiano nje ya mazingira rasmi ya kazi.

/ Published posts: 1215

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram