135 views 3 mins 0 comments

WITO WATOLEWA WAKULIMA KUCHANGAMKIA FURSA ZINAZOTOLEWA KUPITIA WIZARA YA KILIMO

In BIASHARA
August 29, 2024

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

 Elimu ya Matumizi sahihi ya mbolea na usajili wa wakulima vyawavutia wakulima Katavi

Wakulima nchini wametakiwa kuzingatia kanuni bora za kilimo ikiwa ni pamoja na kuzingatia matumizi sahihi ya mbolea kwenye shughuli zao za kilimo.

Aidha, wakulima wametakiwa kuacha kilimo cha mazoea na kufuata kanuni bora za kilimo ikiwa ni pamoja na kutumia mbolea kwa usahihi.


Wito huo umetolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Albert Msovela aliyezungumza  kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Mwanamvua Mrindoko aliyekuwa kwenye majukumu mengine wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Kilimo ni Mbolea mkoani humo tarehe 28 Agosti, 2024.


“Niwasihi wakulima wote nchini wakiwemo wa mkoa huu wa Katavi kuchangamkia fursa zinazotolewa kupitia sekta ya kilimo ili muweze kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali ya Jemedari Dkt. Samia Suluhu Hassan” Msovela ameongeza.


Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Eliurd Mwaiteleke amesema, matumizi ya mbolea kwa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ni zaidi ya asilimia 75 ya mbolea zote zinazoingizwa nchini na kuzalishwa na viwanda vya ndani.


Amesema, mikoa inayoongoza kwa matumizi ya mbolea katika kanda hiyo ni pamoja na Mikoa ya Ruvuma, Mbeya, Songwe, Njombe, Iringa, Rukwa na Katavi.
Ameongeza kuwa, kwa msimu wa kilimo 2023/2024 jumla ya wakulima 14,677 kati ya wakulima 69,073 waliosajiliwa katika mfumo wa ruzuku ikiwa ni sawa na asilimia 21.2 walinunua mbolea za ruzuku kiasi cha tani 4,097.75 zenye thamani ya ya ruzuku kiasi cha shilingi bilioni 4.5.


Amesisitiza kuwa, Serikali imekuwa ikisisitiza matumizi sahihi ya mbolea ili kuwafanya wakulima walime eneo dogo na kuvuna mazao mengi kwani ongezeko la watu duniani linapunguza eneo ambalo lingeweza kutumika kwa shughuli za kilimo.


Mwaiteleke alimalizia kwa kuuomba uongozi wa Mkoa wa Katavi na wadau wa kilimo kuunga mkono kampeni ya Kilimo ni Mbolea ili kuwaeleimisha wakulima na kuwahamasisha kuondokana na kilimo cha mazoea kisichokuwa na tija ili waweze kujikwamua kiuchumi.

Kwa upande wake mkulima wa mahindi, Frenk kibigas ameishukuru Serikali ya Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa kuweka nguvu kwenye sekta ya kilimo kwa kutoa ruzuku ya mbolea na kuwezesha upatikanaji wa vipimia udongo ili kuwafanya wakulima kutumia mbolea sahihi kulingana na mahitaji ya udongo na hivyo kuongeza uzalishaji

Chiku Mlisho ni mkulima wa mahindi  mwenye shamba lenye ukubwa wa ekari 4 katika kijiji cha Igalula, Mpanda Ndogo, wilayani Tanganyika ameeleza kufurahishwa na  huduma ya kuhuisha taarifa zake zitakazo muwezesha kupata mbolea ya ruzuku msimu ujao baada ya kuongeza ekari ukubwa wa shamba kutoka ekari 4 hadi 6 na hivyo kukuza uchumi wake.

/ Published posts: 1486

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram