101 views 2 mins 0 comments

NCHIMBI:CCM ITAENDELEA KUWA SAUTI YA WASIO NA SAUTI

In KITAIFA
August 11, 2024

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

_Asema viongozi mabingwa wa upinzani, walio waadilifu wataendelea kurejea CCM mmoja baada ya mwingine_

_Ziara yake yamng’oa Katibu wa Chadema Kagera na mamia wengine*
_

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amesema chama hicho kitaendelea kuwa sauti ya wasio na sauti.

Balozi Nchimbi amesema kuwa viongozi na wawakilishi wanaotokana na CCM, lazima wawe wanyenyekevu, waadilifu na wanaoguswa na hali ya Watanzania hasa kuhusu maslahi na haki zao.

Katibu Mkuu wa CCM huyo amesema hayo Jumamosi Agosti 10, 2024 alipokuwa akizungumza na Wanachama wa CCM, pamoja na  wananchi wa Bukoba Mjini kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Mayunga, mjini Bukoba.

Balozi Nchimbi alifafanua kuwa kazi ya CCM ni kutetea wanyonge na kwamba mtu akionewa au kunyanyaswa, sehemu ya kwanza kukimbilia iwe CCM.

Balozi Nchimbi ametumia nafasi hiyo kuipongeza Serikali Mkoa wa Kagera na Chama Cha Mapinduzi mkoani humo, kwa usimamizi mzuri wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020 – 2025.

Aidha, alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa Shilingi Trilioni 12 kwa ajili ya miradi mbalimbalo ya maendeleo Mkoa wa Kagera na kusema ile dhana ya mkoa huo kuwa mojawapo ya mikoa ya pembezoni, inaondoka.

Katika hatua nyingine Balozi Nchimbi, amewaambia Watanzania kwamba wanasiasa ‘mabingwa’ na waadilifu walio vyama vya upinzani, wote wataendelea kuwaona mmoja baada ya mwingine, wakirejea CCM.

Alisema maneno hayo baada ya kumpokea aliyekuwa Katibu wa Chadema Mkoa wa Kagera, Ndugu Danstani Mtagayiwa, aliyerejea CCM kutoka Chadema, pamoja na mamia ya waliokuwa wanachama wa chama hicho cha upinzani.

Balozi Nchimbi ameendelea na ziara yake ya siku sita mkoani Kagera yenye lengo la  kusikiliza kero mbalimbali za wananchi, kuangalia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na kuimarisha uhai wa Chama cha Mapinduzi.

Katika ziara hiyo Balozi Dkt.Nchimbi  ameambatana na Ndugu Issa Haji Usi Gavu, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) – Oganaizesheni, Ndugu Amos Gabriel Makalla, Katibu wa NEC – Itikadi, Uenezi na Mafunzo na Ndugu Rabia Abdalla Hamid, Katibu wa NEC – Siasa na Uhusiano wa Kimataifa.

/ Published posts: 1491

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram