58 views 2 mins 0 comments

WAKILI NKUBA: UCHAGUZI URAIS TLS UMEHUJUMIWA

In KITAIFA
August 03, 2024

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

*Apinga matokeo mahakamani

ALIYEKUWA urais wa Chama Cha Mawakili Tanganyika (TLS), Wakili Sweetbert Nkuba ametangaza kupinga matokeo mahakamani yaliyompa ushindi Wakili Boniface Mwabukusi huku akitaja sababu mbalimbali anazodai zimehujumu uchaguzi huo.

Akizungumza jana jijini Dodoma, Wakili Nkuba alisema hakubaliani na matokeo hayo na anapingaย  matokeo yaliyotangazwa na Kamati ya uchaguzi ya TLS kwasababu si matokeo yanayoakisi uchaguzi uliofanyika.

“Kuna uchakachuaji mkubwa sana umefanyika, Kamati ilikuwa ikijua idadi ya wapigakura wakati ikiandaa karatasi za kura lakini katika hali ya kushangaza na isiyo ya weledi.”

“Kamati ilishiwa karatasi za kupigia kura na Kamati ikachukua jukumu la kwenda kuchapisha karatasi nyingine katikati ya zoezi la uchaguzi, mnaweza kuona Kamati ilikuwa haijajipanga ama kwa makusudi au kwa kuamua kuhujumu jitihada ambazo tulikuwa tumezifanya katika kujiandaa na uchaguzi,”alisema.

Pia alisema walipeleka mawakala wa kuhesabu kura na makubaliano ilikuwa kwa namna yeyote wasipewe vifaa vya mawasiliano lakini katika hali ya kushangaza na yakustaajabisha matokeo yalianza kurushwa mitandaoni kabla ya kutangazwa na kamati ya uchaguzi.

“Wameanza kupongezana mitandaoni wakimpongeza mtu anayesadikika kuwa ni mshindi kabla matokeo rasmi hayajatangazwa na Kamati, matokeo yametangazwa masaa mawili kabla, na mshindi ameanza kupongezwa kwa maandiko mbalimbali kabla ya Kamati ya uchaguzi kutoa matokeo, tunaamini mawakala na watu wote waliokuwa kwenye chumba Cha kuhesabu kura hawakuwa na namna yeyote ya mawasiliano,”alisema.

Alisema uchaguzi huo umehujumiwa kutokana na Kamati kukosa weledi na kuhusika kuunajisi mchakato wa uchaguzi huo.

“Napenda kuujulisha umma ninakwenda mahakamani nimewaelekeza Mawakili wangu kwenda kupinga matokeo na kubatilisha ushindi uliotangazwa na Kamati ya uchaguzi,”alisema.

Wakili Nkuba alisema Mahakama ndio sehemu yenye haki na anaamini itasimamia haki na kuufuta uchaguzi huo na kuitisha uchaguzi mpya kwa ajili ya kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa viwango na kwa kuzingatia weledi na usawa wa pande zote.

/ Published posts: 1209

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram