51 views 3 mins 0 comments

WANANCHI WAIOMBA SERIKALI KUTOA ELIMU ZAIDI YA HOMA YA INI

In KITAIFA
July 29, 2024

Na Anton Kiteteri



Wakati Dunia inaadhimisha Siku ya Homa ya Ini wananchi wamelalamikia kukosekana kwa elimu juu ya ugonjwa huo, hali ambayo inasababisha watu wengi kushindwa kufahamu namna ya kujikinga.

Wananchi hao wanasema kukosekana kwa elimu kunasababisha wengi wao kuchelewa kugundua na kutibu ugonjwa na kuufanya usambae na kusababisha ongezeko la maambukizi. Pia wananchi wengi wanashindwa kufahamu namna ya kujilinda dhidi ya ugonjwa huo.

Veronica Sando kutoka mkoani Mara ameiomba serikali kupeleka elimu kuhusiana na homa ya Ini katika maeneo ya vijijini ili kusaidia wananchi kufahamu ugonjwa huo na namna ya kujikinga.

“Ugonjwa wa ini kwakweli siwezi kusema kama nina elimu nao isipokuwa nasikia tu kwamba kuna ugonjwa wa ini na matatizo yake ni makubwa sana, wito wangu kwa serikali ni kwamba ijaribu kupeleka elimu hii chini hasa kwa wananchi walioko vijijini wasiotambua elimu hii na wasiofahamu kwamba kuna ugonjwa kama huu.” alisema Sando

Elichilia Shayo mtaalamu wa magonjwa ya ndani kutoka Hospitali ya KCMC mkoani Kilimanjaro, amesema ili kusaidia kupunguza changamoto ya maambukizi ya ugonjwa huo, serikali na wadau wanapaswa kutengeneza mfumo ambao utasaidia kuongeza wigo wa utoaji wa chanjo katika maeneo ya vijijini.

“Kwa wale ambao wapo kwenye kaya ambazo hazina kipato cha kupata hata milo miwili au mitatu kwa siku, kunahitajika msaada kupitia programu mbalimbali ambazo zinahusisha pia mashirika mengine yasiyo ya kiserikali. Pengine ingesaidia kuongeza wigo wa watu kupata chanjo ili baadaye tuwe na wananchi ambao hawana virusi vya homa ya ini aina ya B.”aliongeza Shayo.

Hata hivyo Dkt. Salimu Ismaili kutoka Hospitali ya Mkoa Geita ameitaka serikali kuongeza juhudi katika utoaji wa elimu kuhusu ugonjwa huo, huku akishauri serikali kutumia njia za mawasiliano na mitandao ya kijamii kuhakikisha kwamba elimu inawafikia wananchi kiurahisi.

“Inabidi sasa kutengenezwe namna ambayo serikali inaweza kutumia vyombo vya mawasiliano kufikisha elimu kuhusiana na ugonjwa huu. Watu wengi wanashindwa kuuelewa kwa sababu ni ugonjwa ambao unaingia taratibu na unachukua kipindi kirefu mpaka mgonjwa anakuja kupata tatizo. Kwa hiyo, wengi wanakuwa hawafahamu ugonjwa huu.” alisema Dkt Ismaili.

Kauli mbiu ya siku ya homa ya Ini duniani kwa mwaka 2024 inasema “Ni wakati wa kuchukua hatua. Pima, Chanja, Pata tiba” ikiashiria umuhimu wa kuchukua hatua za haraka na za makusudi katika kupambana na homa ya ini ili kupunguza athari za ugonjwa huo.

/ Published posts: 1214

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram