189 views 2 mins 0 comments

TANZANIA KUWA MWENYEJI WA KONGAMANO LA OILI LA UMOJA WA MATAIFA KUHUSU UTALII WA VYAKULA VYA ASILI BARANI AFRIKA

In KITAIFA
July 27, 2024



Na Mwandishi Wetu- Zimbabwe

Tanzania inatarajiwa kuwa Mwenyeji wa Kongamano la Pili la Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UN Tourism), Kanda ya Afrika kuhusu utalii wa vyakula vya asili katika Bara la Afrika kwa mwaka 2025.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UN Tourism), Zurab Pololikashvili katika ufunguzi wa Kongamano la kwanza la Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani, Kanda ya Afrika kuhusu Utalii wa vyakula vya asili katika Bara la Africa (Gastronomy) linaloendelea jijini Victoria Falls nchini Zimbabwe leo Julai 26, 2024.

Bw. Pololikashvili amemshukuru Waziri wa Maliasili na Utalii wa Tanzania, Mhe. Angellah Kairuki kwa ushirikiano wake na nia yake ya kutaka kutangaza utalii wa chakula na kusisitiza kuwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani liko tayari kutoa ushirikiano kwa nchi za Afrika katika kutangaza utamaduni wa Kiafrika hasa Utalii wa vyakula.

“Afrika sio tu kwa ajili ya safari na kuangalia mazingira ya asili, bali pia tunataka kuuonesha ulimwengu kwamba Afrika ni tajiri katika utamaduni hasa utalii wa vyakula ambao ni sehemu kubwa ya utamaduni wetu” alisisitiza.

Naye, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amesema kufanyika kwa Kongamano hilo  nchini Tanzania  kutakuwa na manufaa makubwa katika kukuza mnyororo mzima wa thamani katika utalii ikiwemo Utalii wa vyakula hasa kugusa wadau wengi wakiwemo wakulima wafugaji, wavuvi,wazalishaji wa nafaka,wachakataji wa mafuta n.k.

“Tunao mwaka mmoja wa kufanya maandalizi na tutajipanga vizuri kuhakikisha kwamba Tanzania inaonesha urithi na utajiri mkubwa tulionao lakini ni nafasi nzuri katika kukuza utalii wetu zaidi” Mhe. Kairuki ameongeza.

Amefafanua kuwa kupitia jukwaa hilo kutakuwa na mashindano mbalimbali kwa ajili ya ubunifu  na wenye vyuo na wataalamu wengine watapata nafasi ya kubadilishana uzoefu na wenzao kutoka nchi nyingine za Afrika.

Kongamano hilo limefunguliwa rasmi na Rais wa  Jamhuri ya Zimbabwe, Mhe. Emmerson Mnangagwa ambaye amesisitiza juu ya umuhimu wa Sekta ya Kilimo katika kukuza Utalii wa Chakula.

/ Published posts: 1214

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram