288 views 3 mins 0 comments

MWABUKUSI KUACHIWA HURU ASHINDA KESI,AJA KUJIPANGA UPYA KUGOMBEA URAIS TLS

In KITAIFA
July 26, 2024

Na Antonio Kiteteri WAMACHINGA DAR ES SALAAM

Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Dar es Salaam,imetoa hukumu ya kesi iliyokuwa imefunguliwa na Wakili wa kujitegemea Boniface Mwabukusi dhidi ya TLS (Chama cha Mawakili Tanganyika) kupinga kuondolewa kwake kugombea nafasi ya urais ndani ya Chama hicho cha mawakili nchini katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao.

Baada ya mahakama kusikiliza hoja za pande zote mbili imeridhika na hoja zilizotolewa na upande wa waleta hoja  ambapo rasmi mahakama imetengua maamuzi ya kamati ya rufani ya TLS, hivyo kumpa Wakili Mwabukusi nafasi ya kuwa mmoja wa wagombea kwenye nafasi ya urais wa TLS.

Steven Mwakibolwa wakili wa kujitegemea na aliyekuwa anaiwakilisha TLS akizungumza na waandishi wa habari baada ya mahakama kutangaza uamuzi huo wa kumrejesha Mwambukusi kwenye kinyang’anyiro  hicho cha urais wa TLS,ameeleza kuwa wao  TLS hawakuwa na pingamizi lolote dhidi ya mleta hoja kwa kuwa ni haki yake ya msingi na kikatiba, hivyo uamuzi wa mahakama umefuata mkondo wa haki kulingana na maombi ya mleta hoja.

Kwa upande wake Wakili Mwambukusi amewashukru wale waliosimama nae mpaka haki kupatikana.Pia Mwambukusi ameelezea kufurahishwa na namna mahakama ilivyotoa maamuzi kwa haraka,wakati na kwa haki.

“Kwanza nachukua nafasi hii kumshukru Mungu kwa haya yote yaliyojiri,namshukru Mungu kwa ajili ya mawakili wangu, namshukru Mungu kwa ajili ya mahakama, namshukru Mungu kwa ajili ya mawakili wote ambao hawakukata tamaa,waliendelea kupiga kelele dhidi ya dhuruma,kwa sababu niliondolewa kwa dhuruma,Kwa uonevu na kwa ubabe”, Alieleza Wakili Mwambukusi.

“Wakati nikifanyiwa haya sikuamini kama hawa ni mawakili wenzangu,kwa umri waliokuwa nao na vitendo walivyokuwa wakinifanyia ni vitendo ambavyo kwa kweli vilinikwaza lakini nilijua haki ipo na  nashukuru mawakili wangu walifanya kazi usiku na mchana na nashukuru mahakama imetusikiliza kwa haraka sana,hili ni jambo ambalo linanitia Moyo”, Alifafanua Wakili Mwambukusi.

Mwambukusi ameeleza kuwa yeye ni Simba anayetegemea kuongoza kundi la Simba Kwa kuamini kwamba hakuna kondoo ndani ya Chama hicho na kufafanua kuwa watanzania wataanza kupata ladha ya uwepo wa Chama Cha Mawakili Tanganyika.Ameahidi kuifanya TLS kuwa moja na yenye ushirikiano.

Mwanzo wakati wa mchakato wa kuwapata wagombea wa nafasi ya urais,Wakili Mwambukusi alienguliwa kugombea nafasi hiyo ndani ya Chama Cha Mawakili Tanganyika (TLS), na kamati ya rufani ya TLS.

/ Published posts: 1480

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram