122 views 3 mins 0 comments

TANZANIA, MAREKANI NA INDIA KUONGEZA USHIRIKIANO KATIKA SEKTA YA NISHATI

In KITAIFA
July 17, 2024

Na Mwandishi wetu WAMACHINGA

Dkt.Mataragio azindua programu ya ushirikiano ya TriDEP

Inalenga kuongezea Wataalam uwezo katika eneo la Nishati Jadidifu

TriDEP kugusa pia uimarishaji wa Gridi ya Taifa*


Serikali ya Marekani, India na Tanzania zimekubaliana  kuongeza ushirikiano katika   miundombinu ya  umeme unaotokana na Nishati Jadidifu ili iweze kuchangia ipasavyo katika gridi ya Taifa kama ilivyo kwa vyanzo vingine vya Nishati kama vile Maji na Gesi Asilia.



Hayo yameelezwa leo Julai 17, 2024 jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu,  Wizara ya Nishati, Dkt. James Matarajio wakati wa uzinduzi wa Programu ya TriDEP inayolenga kuboresha ushirikiano katika sekta ya Nishati Jadidifu na Nishati Safi ya Kupikia hapa nchini.

Aidha, ushirikiano huo unalenga kuwajengea uwezo Wataalam wa Kitanzania kuhusu masuala ya Nishati Safi na Jadidifu nchini.



Dkt.Mataragio amesema kuwa,  nchi za Marekani na India zimepiga hatua kubwa katika masuala ya Nishati Safi ya Kupikia na Jadidifu na hivyo Tanzania imeamua kuimarisha ushirikiano na mataifa hayo katika kipindi hiki ambacho Taifa linaendeleza kampeni ya matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.

“Ushirikiano huu wa kipekee ni wa kwanza katika bara la Afrika unaotekelezwa na Shirika la USAID na The Asia Foundation ambao utawezesha wataalam kutoka Vyuo vya elimu ya Juu, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wakala wa Nishati Vijijini (REA), EWURA na TAREA kujifunza kwa kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya nishati nchini India.



Ameongeza kuwa, ushirikiano huo utasaidia katika kupata njia madhubuti za kutatua changamoto zinazojitokeza katika mifumo ya gridi hapa nchini.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkazi wa USAID Tanzania, Alexander Klaits amesema lengo la ushirikiano huo ni kukuza masuala ya nishati nchini kwa kuwa Tanzania inapiga hatua kubwa katika kuimarisha upatikanaji wa nishati kwa wananchi.



“Ushirikiano huu utaimarisha uwezo wa ndani na kuongeza fursa za kibiashara kati ya kampuni za Marekani nchini Tanzania. Tunayo heshima kushirikiana na India kusaidia Tanzania iendelee kuimarisha sekta ya nishati katika kanda ya Afrika Mashariki.”  Amesema Klaits.

Aidha, Balozi Mdogo wa India nchini, Manoj Verma amesema “ni  jambo la kujivunia kuona ushirikiano wa kwanza kati ya India na Marekani katika Bara la Afrika unaanzia kufanyika nchini Tanzania na ushirikiano huu unatoa mfano bora wa kimkakati kati ya Tanzania na India kwa kuzingatia maendeleo ya Nishati Jadidifu.”



Amesema Ushirikiano huo utaongeza nguvu katika kipindi ambacho Tanzania inaelekea  kukamilisha miradi mikubwa ya nishati na kuiunganisha kwenye gridi ya Taifa.

Naye, Kaimu Kamishna Msaidizi wa Nishati Jadidifu, Wizara ya Nishati, Mha. Imani Mruma amesema kuwa Tanzania inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya Nishati Jadidifu ukiwemo mradi wa umeme Jua uliopo Kishapu mkoani Shinyanga utakaozalisha megawati 150, miradi ya Joto Ardhi na miradi mingine ya upepo ambayo ipo katika hatua mbalimbali za upembuzi yakinifu.

/ Published posts: 1215

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram