Na Mwandishi wetu WAMACHINGA
Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imepokea taarifa ya Utafiti wa Madini ya Dhahabu unaofanywa na Kampuni ya Twiga Corporation Limited inayomilikiwa kwa ubia kati ya Serikali kwa asilimia 16 na Kampuni ya Barrick Tanzania Limited kwa asilimia 84 ikiwa ni utaratibu kwa Serikali kupokea taarifa za maendeleo ya utafiti kutoka kwa kampuni za uchimbaji madini kila baada ya Robo Mwaka.
Akitoa wasilisho hilo, Mjiolojia kutoka Barrick Bw. Muganyize Byemelwa amesema Barrick inaendelea na utafiti wa madini katika maeneo ya leseni wanazomiliki kwa lengo la kupanua wigo wa uchimbaji na kuisha maisha ya mgodi.
Naye, Mjiolojia mwandamizi kutoka GST Bw. Muhudi Ngerezi ametoa wasilisho kuhusu historia ya GST, kazi zinazo tekelezwa na taasisi hiyo ikiwemo shughuli za utafiti wa njia ya Jiolojia, Jiofizikia, Jiokemia na kuelezea shughuli za maabara zinazofanywa na taasisi hiyo.
Aidha, Meneja wa Sehemu ya Jiolojia Bw. Maswi Solomon akitoa neno la shukrani la kuhitimisha amesema GST ndiyo kitovu cha taarifa za tafiti za madini nchini ikiwemo kuzihakiki hivyo ameisihi Kampuni ya Barrick kuendelea kutoa taarifa za utafiti zinazofanywa na Kampuni hiyo kila baada ya Robo Mwaka kama Sheria ya Madini inavyowataka. Huku akisema kazi hiyo inairahisishia GST kuzihakiki kwa kuwa mambo mengi yenye dukuduku yanakuwa yanatolewa ufafanuzi wakati wa wasilisho.
Pamoja na mambo mengine, Meneja wa Utawala na Rasilimaliwatu wa GST Jacqueline Kaluwa ameiomba Kampuni ya Barrick kuwapa fursa Wataalamu kutoka GST kujifunza teknolojia mbalimbali za utafiti kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wa Wataalamu hao hasa kwenye nyanja ya ukadiriaji mashapo.
Awali, Mkurugenzi wa Huduma za Jiolojia Dkt. Ronald Massawe wakati akitoa neno la ufunguzi alieleza chimbuko la uwasilishwaji wa taarifa za utafiti za Barrick huku Mtendaji Mkuu wa GST Dkt. Mussa Budeda aliwakaribisha Wataalamu wa Kampuni ya Barrick kuendelea na utaratibu wa kuwasilisha ripoti ya shughuli za utafiti zilizofanyika na zinazoendelea kufanyika katika migodi ya uchimbaji madini ya dhahabu ya Barrick kwa wakati sahihi.