128 views 2 mins 0 comments

WAZIRI MKUU: MATOKEO YA SENSA YANAPASWA KUWAFIKIA NGAZI YA MIKOA NA HALMASHAURI

In KITAIFA
July 02, 2024

Na Mwandishi wetu WAMACHINGA LINDI

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema matokeo ya sensa yanapaswa yawafikie watendaji na walengwa wote katika ngazi ya mkoa na Halmashauri na yawe msingi wa rejea katika kufanya maamuzi yote ya kibajeti, kupanga miradi ya maendeleo na kufuatilia utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya kisekta.


Ametoa agizo hilo leo Julai 2, 2024 wakati akizungumza na viongozi, wananchi na wadau mbalimbali waliohudhuria ufunguzi wa Mafunzo ya Matumizi ya Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 kwa Viongozi na Watendaji wa Halmashari za Wilaya za Liwale, Nachingwea na Ruangwa mkoani Lindi uliofanyika kwenye viwanja vya Maonesho, Kilimahewa mjini Ruangwa.

Amesema usambazaji na mafunzo ya matumizi ya matokeo ya sensa viwe ni ajenda ya kudumu katika vikao vyote vya kikanuni katika ngazi ya Mkoa na Halmashauri.


“Watendaji wote myabebe haya matokeo mkayatumie, muwe viongozi wa kuhakikisha yanatumika,”amesema.

Amewataka viongozi na watendaji wakae pamoja na kutafakari namna bora ambayo matokeo ya sensa yanaweza kutumika kubadili hali za maisha ya wananchi pamoja na kuhimiza uwekezaji.

“Matokeo haya yanapaswa yatumike na yasaidie kubadilisha maisha ya wananchi huku mkijua kwamba fedha nyingi zimetumika kuifanya kazi hiyo,” amesema.


Akitolea mfano Mkoa wa Lindi, Waziri Mkuu ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa amesema: “Mkoa wa Lindi una fursa nyingi za kuvutia uwekezaji hivyo ni wakati sasa wa kutumia matokeo haya ya sensa kuitangaza Lindi na kuibadili kupitia uwekezaji,”

Amewataka viongozi hao waifanye kazi ya kuhuisha anwani za makazi na kuweka mikakati ya kutunza miundombinu yake kuwa ni endelevu kwa ajili ya kurahisisha ufikiwaji wa wananchi, kurahisisha biashara mtandao, uwekezaji na uwajibikaji.

“Kila Halmashauri nchini, ifanye uhakiki wa vibao vilivyowekwa, waelimisheni wananchi umuhimu wake na pia wasiving’oe kwa sababu vinasaidia kuelekeza hata akija mgeni kwa mara ya kwanza hahitaji kuelekezwa na mtu au kuulizia kwa mtu anakokwenda,” amesisitiza.


Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande amesema Tanzania imekuwa mfano wa kuigwa kwenye ufanyaji wa sensa ya watu na makazi kwa njia ya kidijitali na akasisitiza kuwa watendaji wa Kata na Tarafa watumie ipasavyo matokeo ya sensa kupanga mipango ya maendeleo na waandae zana na ufuatiliaji na tathmini yanayotokana na matokeo ya sensa kwa sababu yanapimika.

/ Published posts: 1480

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram