56 views 26 secs 0 comments

MAREKANI,UINGEREZA ZALAANI UTEKAJI NYARA NA MAUAJI YA WAANDAMANAJI KENYA

In KIMATAIFA
June 26, 2024

Marekani, Uingereza na mataifa mengine yamelaani kutekwa nyara na kuuawa kwa waandamanaji nchini Kenya wakati wa maandamano yanayoendelea ya kupinga Muswada wa Sheria ya Fedha ambayo yamekuwa yakifanyika kote nchini.

Katika taarifa ya pamoja, Mabalozi na Makamishna Wakuu kutoka nchi 13 walielezea wasiwasi wao juu ya ghasia zinazoshuhudiwa kote nchini na kusababisha vifo.

“Tunasikitishwa sana na ghasia zilizoshuhudiwa katika maeneo mengi ya nchi wakati wa maandamano ya hivi majuzi, na tumeshtushwa hasa na matukio yanayoshuhudiwa nje ya Bunge la Kenya,” ilisema taarifa hiyo

Wakijiita “marafiki na washirika wa Kenya”, mabalozi hao walisema kuandamana ni haki ya kikatiba.

“Tunatambua kwamba katiba ya Kenya inahakikisha haki ya kuandamana kwa amani. Wahusika wote wana wajibu wa kuheshimu, kudumisha, kukuza na kutimiza kanuni za demokrasia na utawala wa sheria, hasa kwa kuhakikisha mwitikio sawia wa usalama.”

Pia walitoa wito wa ushirikishwaji wa kiraia na Wakenya wote “katika kushughulikia masuala muhimu ya umma.

“Tunatoa wito wa kujizuia kwa pande zote, na kuwahimiza viongozi wote kutafuta suluhu za amani kwa njia ya mazungumzo yenye kujenga,” ilisema taarifa hiyo ya pamoja.

/ Published posts: 1214

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram