68 views 2 mins 0 comments

KATIBU MKUU NISHATI AKUTANA NA WAFANYAKAZI

In KITAIFA
June 19, 2024

Na Mwandishi wetu WAMACHINGA

📌 *Ahimiza umuhimu wa ushirikishwaji wa Wafanyakazi*

📌 *Awataka Wakuu wa Idara na Vitengo kutoa fursa  kwa Maafisa*

📌 *Asisitiza motisha kwa wanaofanya vizuri*

📌 *Dkt. Mataragio asisitiza ushirikiano na kuzingatia muda*

Katibu Mkuu wizara ya  Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba  leo 18 Juni, 2024 amekutana na  Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati  ili kujadili mafanikio ya Wizara  yaliyopatikana katika kipindi cha miaka sita, kusikiliza changamoto mbalimbali za Wafanyakazi na utatuzi wake.

Katika kikao hicho kilichofanyika jijini Dodoma, Mramba amesema ni vyema Wakuu wa Idara na Vitengo wakahakikisha wanawapa fursa wafanyakazi wao ili kuwajengea uwezo kwenye utendaji wao wa kazi.

‘Kiongozi mzuri ni yule anayeruhusu wengine kukua na kuwatengeneza watu wake  kwa kutoa fursa nao waweze kukua hivyo nawasisitiza  msiogope  kuwatengeneza maafisa wenu.” Amesema Mramba

Aidha, amewataka Wakuu wa Idara na Vitengo
kuhakikisha  kuwa wanatoa motisha kwa wafanyakazi waliofanya kazi vizuri ikiwemo ya  kuwatambua ili kuongeza ufanisi kwenye utendaji kazi na kuagiza kuwa utaratibu huo uanze mara moja.

Vilevile,  amewataka Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati kuheshimu kazi zao na wazifanye kwa bidii kwani ndizo zinazowabeba.

Kwa upande wake,  Naibu Katibu Mkuu  Wizara ya Nishati,  Dkt. James Mataragio amewataka Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati kuhakikisha  wanafanya kazi kwa ushirikiano  ili kuongeza ufanisi hasa katika utekelezaji wa miradi ya nishati.

‘’ Pia niwasisitize wafanyakazi wenzangu tuwe wepesi  kwenye kujifunza  maana unapojifunza unaongeza ufanisi na pia tuzingatie muda kwenye utendaji kazi ili kuleta tija.” Amesema Mataragio

Akıtoa ufafanuzi juu ya masuala mbalimbali yanayohusu utawala,  Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu,  Bi.Ziana Mlawa amesema  jengo la Wizara ya Nishati katika Mji wa Serikali Mtumba sasa
limefikia asilimia 78.07 ambapo kwa sasa liko kwenye ukamilishwaji na hadi kufikia Septemba mwaka huu  mkandarasi anatarajiwa  kukabidhi jengo hilo.

Amesema kwa sasa Wizara ya Nishati ina jumla ya Wafanyakazi 211 ambapo ametumia fursa hiyo kuwakumbusha  wafanyakazi kuhusu  kutumia vyema mfumo wa upimaji utendaji kazi PEPMIS  kwa wakati.

/ Published posts: 1214

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram