46 views 5 mins 0 comments

RAIS SAMIA KUTUA KESHO KOREA ,MIKATABA SABA KUSAINIWA

In KITAIFA
May 29, 2024

Na Mwandishi wetu WAMACHINGA

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa na ziara ya kikazi  itakayofanyika Jamhuri ya Korea tarehe 30 Mei hadi tarehe 06 Juni 2024.

Katika ziara hiyo,  Rais Samia anatarajia kufanya mambo makuu mawili ambapo Tarehe 2 Juni 2024 atakutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Korea Mheshimiwa Yoon Suk Yeol, na Tarehe 4 hadi 5 Juni, 2024 atashiriki katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kati ya Korea nan chi za Afrika.

Akizungumza na waandishi wa Habari Jana Jijini Dar es Salaam,  Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba alisema Mkutano huo ni wa kwanza kufanyika katika ngazi ya Wakuu wa Nchi na Serikali, ambapo hapo awali Mikutano kama hiyo ilikuwa katika ngazi ya Mawaziri na Wataalamu.

Alisema, akiwa nchini Korea,  Rais Samia atashiriki mikutano miwili ambayo ni Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Korea na Afrika na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Sekta Binafsi ambapo Rais atahutubia katika sehemu ya tatu (3) inayozungumzia Kuimarisha Usalama wa Chakula na Madini โ€œStrengtherning Food and Minerals Security.

Waziri Makamba alisema katika ziara hiyo kutakuwa na  Kusainiwa kwa Hati za Makubaliano Saba ambayo yatahusu Mkataba wa Tamko la Kuingia EPA; Framework Agreement ya EDCF; Mkataba wa Madini ya Kimkakati; Mkataba wa Kutambuliana Vyeti vya Mabaharia; Mkataba wa Uchumi wa Buluu; Mkataba wa KIGAM na GST; na Mkataba kati ya STAMICO na KOMIR.

Pia alisema kutakuwa na Kusainiwa kwa tamko la Pamoja la Mawaziri la kuanza Majadiliano ya Ushirikiano wa Kiuchumi (Joint Ministerial on the Launch of the Negotiation on Economic Partnership Agreement-EPA).

Pia Waziri Makamba alisema “Katika ziara hiyo wanatarajia kufungua soko la ajira kwa Watanzania nchini Korea kwakuwa Korea inachangamoto ya nguvu kazi inayotokana na sababu tatu ambazo ni kuzeeka kwa nguvu kazi iliyopo, kushuka kwa idadi ya vizazi vipya; na vijana kutokutaka kufanya kazi Za shuruba na misuli wanazoziita 3D kwenye sekta ya viwanda, miundombinu, kilimo, uvuvi na ujenzi wa meli.

Kuvutia wawekezaji wa Korea ili wawekeze katika soko la sanaa la Tanzania kwa mustakabali wa kutengeneza ajira kwa vijana kupitia sanaa. Kuiomba Serikali ya Korea kuendelea kutoa mafunzo ya kukuza ujuzi na teknolojia ya wasanii wa Tanzania.” Alisema

Kadhalika Waziri Makamba alisema katika ziara hiyo wanatarajia Kuanzisha ushirikiano na Kituo cha Ushirikiano wa Kimataifa na Maendeleo wa Chuo Kikuu cha Korea Aerospace University (KAU utakaosaidia kuboresha soko la usafiri wa anga, uendeshwaji wa biashara ya usafiri wa anga na uendeshwaji wa utaratibu wa viwanja vya ndege, utaalam, utafiti na huduma.

Waziri Makamba alisema wanatarajia pia Kuwakaribisha Korea kushirikiana na Tanzania katika kufanya utafiti wa kutambua aina ya madini yaliyopo (survey) ambapo kwa sasa ni asilimia 16 tu ndiyo iliyotafitiwa.

Vilevile, Rais Samia atakaribisha wawekezaji kuwekeza katika uchakataji wa madini (beneficiation) na kushirikiana na serikali katika kujenga Kinu cha Uchenjuaji (Smelter) na kiwanda cha siku za baadaye kama wanavyofanya Vietnam na Indonesia.

Kuhusu malengo ya ziara hiyo, Waziri Makamba alisema, wataimarisha ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Jamhuri ya Korea.

Alisema ziara hiyo itafungua zaidi milango ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Korea na kuchochea zaidi ukuaji wa biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo na kufungua milango kwa sekta binafsi ya Korea nchini Tanzania.

Pia alisema katika Ziara hiyo wanatarajia itakuwa chachu na kutoa msukumo kwa Wawekezaji kutoka Korea kuja nchini.

“Ushiriki wa Tanzania katika mkutano tajwa unatarajiwa kukuza uhusiano wa kimkakati; kupanua wigo wa biashara na uwekezaji; kutafuta namna chanya ya kukabiliana na changamoto za kimataifa; kutengeneza minyororo ya kimataifa ya usambazaji wa madini na nishati muhimu; na kujenga urafiki wa kudumu.”

Kadhalika, Waziri Makamba alisema ziara hiyo pia itaimarisha ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Jamhuri ya Korea na inategemewa kufungua zaidi milango ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizi mbili kwa kuchochea zaidi ukuaji wa biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo na kufungua milango kwa sekta binafsi ya Korea nchini Tanzania.

/ Published posts: 1214

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram