122 views 3 mins 0 comments

WAZIRI KAIRUKI  NA CHINA KUSHIRIKIANA KATIKA SEKTA YA UTALII

In KITAIFA
May 14, 2024

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA CHINA

MAKUMBUSHO YA CHINA NA TANZANIA KUSHIRIKIANA

Na Mwandishi Wetu-Beijing

Makumbusho ya Taifa  ya China na Tanzania zimekubaliana  kushirikiana katika kubadilishana uzoefu, teknolojia na kuwa na maonesho ya pamoja  kwa lengo  la kuhakikisha kuwa huduma za makumbusho zinakuwa na faida kwa pande zote mbili za nchi hizo.

Makubaliano hayo yamefikiwa katika mazungumzo kati ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) na Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa la China, Gazo Zheng yaliyofanyika kwenye Makumbusho ya China jijini Beijing Mei 14,2024.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Kairuki amesema kwa kuwa Makumbusho ya Taifa la China ina uzoefu wa miaka mingi, ni vyema ikashirikiana na Makumbusho ya Taifa la Tanzania katika dijitali ,kufanya tafiti, kuwa na Maonesho ya pamoja, kuonesha utamaduni na historia ya nchi zote mbili pamoja na kubadilishana uzoefu wa utaalamu katika kutunza na kuhifadhi mikusanyo.
Aidha, Mhe. Kairuki amesema kuwa Tanzania ingependa kujifunza namna ya  kuvutia kizazi cha vijana kinachokua ili kiwe na utamaduni wa kutembelea Makumbusho mbalimbali zilizopo nchini Tanzania.

Amesema  Serikali ya Tanzania kupitia ubalozi wake ulipo jijini Beijing nchini China utahakikisha unafuata taratibu zote za kuwepo kwa  Mkataba wa Makubaliano kati ya makumbusho hizo ili kurasimisha ushirikiano huo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Zheng amesema Makumbusho ya Taifa la China iko tayari kushirikiana na Tanzania katika maeneo yote yaliyopendekezwa.

“Makumbusho ya Taifa la China ina uzoefu mkubwa na ina wataalamu zaidi ya mia moja hivyo ina furaha kushirikiana na Makumbusho ya Taifa la Tanzania hasa katika kuhifadhi mikusanyo, kufanya tafiti, kubadilishana uzoefu na namna ya kuvutia  vijana kuwa na utamaduni wa kutembelea makumbusho” amesema.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, wajumbe wa Kamati ya Rais ya Kuitangaza Tanzania akiwemo Katibu Mkuu, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Fatma Mabrouk, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Anderson Mutatembwa pamoja na maafisa wa taasisi mbalimbali za sekta za umma.

Waziri Kairuki yuko nchini China kwa ajili ya kushiriki katika Maadhimisho ya Miaka 60 ya Kidiplomasia kati ya Tanzania na China pamoja na uzinduzi wa mwaka wa Utalii na Utamaduni na pia uzinduzi rasmi wa filamu ya “Amazing Tanzania” utakaofanyika Mei 15, 2024 jijini Beijing.

/ Published posts: 1480

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram