Na Mwandishi Wetu
Katika kuhakikisha sekta ya kilimo inazidi kukua, serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia imeongeza bajeti ya sekta ya umwagiliaji kutoka shilingi bilioni 46.5 mwaka 2021/22 hadi shilingi bilioni 373.5 kwa mwaka 2023/2024 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umwagiliaji ili kuongeza tija kwa wakulima.
Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe amezungumza hayo wakati wa hafla ya kusaini mikataba ya miradi 20 ya umwagiliaji leo April 30, 2024 mbele ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majiliwa ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika hafla hiyo.
Bashe ameendelea kumshukuru na kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa utashi wake wa kutoa kipaumbele cha kuwekeza katika miradi ya muda mrefu katika eneo la kilimo ikiwemo cha umwagiliaji akisema kuwa mageuzi makubwa yamefanyika kupitia sekta hiyo.
“Sekta ya kilimo imeendelea kufanya mageuzi makubwa na kuwekeza katika maeneo ya msingi ili uongeza uzalishaji na tija, kufanya kilimo kiwe cha kibiashara zaidi na kuongeza pato la wakulima wadogo kwa ajili ya kuboresha maisha yao, kwa kutambua umuhimu huo, Serikali ya awamu ya sita iliongeza bajeti ya sekta ya umwagiliaji kutoka Shilingi bilioni 46.5 mwaka 2021/22 hadi Shiling bilioni 361.5
2022/23 na mwaka 2023/2024 bajeti imeongezeka kufikia bilioni
373.5″ – Aliongeza Mhe. Hussein Bashe, Waziri wa Kilimo
Kwa upande mwingine, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Bw. Raymond Mndolwa ameeleza utekelezaji wa miradi hiyo ulipofikia na ni kwa namna gani Wakulima watanufaika.
Mndolwa amesema kuwa Tume ilipanga kujenga, kukarabati na kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika miradi 780 ndani ya kipindi cha miaka miwili
“Miradi ya umwagiliaji huchukua zaidi ya miezi 18, hivyo kukamilika kwa ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika skimu hizo kwa miaka hii miwili kutaongeza eneo la umwagiliaji zaidi ya hekta 256,000 na kufanya eneo linalomwagiliwa kufikia hekta 983,465.46 sawa na asilimia 81.9 ya lengo la kufikisha hekta 1,200,000 ifikapo 2025 na ongezeko hilo litatengeneza ajira za kudumu takribani 1,352,127” – Amesema Mndolwa