Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amewaondoa Watendaji wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Meneja wa Vivuko Kanda ya Mashariki na Kusini Mhandisi Lukombe King’ombe na Mkuu wa Kivuko cha Magogoni – Kigamboni, Idd Stamili Juma kwenye nafasi zao na kuagiza kupangiwa kazi nyingine kwa kushindwa kusimamia kikamilifu huduma bora kwa wananchi wanaotumia usafiri wa kivuko kati ya Magogoni – Kigamboni.
Waziri Bashungwa ametoa maagizo hayo Mkoani Dar es Salaam leo Aprili 29, 2024 wakati akikagua huduma zinazotolewa na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) na kusikiliza changamoto za wananchi wanaotumia usafiri wa vivuko kati ya Magogoni na Kigamboni na kuonyesha kutoridhishwa na utoaji wa huduma za Wakala huo.
Katika ziara hiyo, Waziri Bashungwa amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Balozi Mhandisi Aisha Amour kupeleka timu mpya ambayo itashirikiana kwa karibu na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma bora za vivuko katika maeneo hayo.
“Nikuagize Katibu Mkuu kuangalia namna ambavyo utawabadilishia mazingira na kuwapa
majukumu mengine Meneja wa Kanda na Mkuu wa Kivuko cha Magogoni – Kigamboni na kuleta Watendeji wapya ambao watamsaidia Mtendaji Mkuu wa TEMESA kusimamia mkakati mpya wa maboresho ya TEMESA”, Amekaririwa Waziri Bashungwa.
Aidha, Bashungwa amemuelekeza Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Lazaro Kilahala kuanza mara moja kufanya maboresho katika majengo ya abiria katika maeneo yote nchini yenye huduma za vivuko, ambapo ameelekeza kuanza kuondoa feni mbovu na kuweka mpya katika eneo la Magogoni – Kigamboni.
“Nimekagua na nimejionea mwenyewe sehemu ya jengo la abiria linahitaji maboresho na usafi, nimeona zile feni kwanza ikiwashwa unakimbia kwa lile vumbi lililopo unaweza ukapata madhara makubwa ya kiafya hivyo zile feni ziondolewe mara moja na nimechukizwa na majibu yaliyokuwa yakitolewa sidhani kama Wizara kupitia TEMESA tunaweza kushindwa mambo madogo madogo kama haya”, Amesisitiza Bashungwa.
Kuhusu changamoto za mfumo wa malipo wa kukatia tiketi wa N-Card, Bashungwa amesema kuwa tayari timu zimeshafanya uchambuzi wa changamoto hiyo na yenyewe Serikali inakwenda kuyafanyia kazi.
Kadhalika, Bashungwa ameagiza TEMESA kuhakikisha wananchi wote wanaopata huduma za vivuko katika eneo la Magogoni na Kigamboni pia wawe wanalipa nauli kama mchango kwa ajili ya kusaidia uendeshaji wa huduma hiyo.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ameeleza kuwa taasisi nyingi zilizopo kwenye Mkoa wake zinafanya kazi kubwa na ameitaka pia TEMESA kuongeza ushirikiano na Mkoa kwa kuwa wao wanajihusisha moja kwa moja na wananchi.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Lazaro Kilahala ameeleza kuwa kwa sasa Kituo cha Magogoni – Kigamboni kina vivuko viwili ambavyo ni MV Kazi na MV Kigamboni vinavyotoa huduma za uvushaji kwa saa 24 na kufafanua kuwa kivuko cha MV Magogoni ambacho kimepelekwa kwenye matengenezo makubwa utekelezaji wake umefikia asilimia 55.2.