129 views 3 mins 0 comments

TARURA KUSHIRIKIANA NA WILAYA YA KINONDONI KUTUNZA MITARO

In KITAIFA
April 18, 2024

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

Dar es Salaam

Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kushirikiana na Wilaya ya Kinondoni wamekutana na kupanga mkakati wa kutunza  mitaro inayojengwa katika barabara Wilayani humo.

Hayo yamebainishwa katika kikao cha pamoja kati ya ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Meneja wa TARURA Mkoa wa wa Dar es Salaam pamoja na Timu ya Kitengo cha Mazingira kutoka TARURA Makao Makuu.

Akiongea katika kikao hicho Meneja wa TARURA mkoa wa Dar es Salaam Mhandisi Geofrey Mkinga ameeleza umuhimu wa utunzaji wa mitaro na barabara kwa ujumla na kusisitiza kuwa jambo hili si la TARURA pekee bali linahusisha uongozi kuanzia ngazi ya wilaya, mitaa na wananchi ambao ndio wanaoshiriki kutupa taka  katika mitaro na kusababisha mafuriko na magonjwa ya mlipuko.

“Zipo sheria zinazohusu utanzaji wa barabara, mazingira na  afya na sheria hizi zipo chini ya usimamizi wa Halmashauri ambapo Wakurugenzi na Wakuu  wa Wilaya ndio wenye jukumu hilo,  hivyo kwa kushirikiana tunaweza kufanikisha vizuri zoezi hili”, alisema.

Aidha, wataalamu wa mazingira wamewasilisha sheria mbalimbali zinazo bainisha sera, sheria na vifungu vinavyoelezea namna ya kutunza mazingira pamoja na adhabu za ukiukwaji wa sheria hizo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Saadi Mtambule ameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha akishirikiana na wasaidizi wake katika kufanikisha zoezi hili.

“Tunashukuru kwa jitahada na ushirikiano mnaoendelea kutupa mara kwa mara, sisi ni serikali na ni wajibu wetu kutunza na kusimamia rasilimali zote za serikali tukishirikiana wadau na wananchi kwa ujumla.

Vilevile ameeleza kuwa wao kama wilaya wanakampeni ya kufanya usafi siku za Jumanne na Alhamisi kuanzia saa 2 hadi saa 3 asubuhi.

“Katika barabara ya Nyota Njema wananchi wamejitolea kuchanga fedha kila mwaka kwa ajili ya usafi na utunzaji wa barabara na katika maeneo mengine wananchi wameendelea kutoa ushirikiano katika kufanya usafi”. Alifafanua Mhe. Mtambule

Mhe. Mtambule aliendelea kusema kuwa Kinondoni ina mikakati ya kushirikiana na wadau kutoka ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha swala la usafi katika wilaya ya Kinondoni inazidi kuwa safi hasa katika maeneo ya mama lishe.

TARURA ipo katika kampeni ya kuhamasisha na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa  kutunza miundombinu ya barabara kwa kuepuka kutupa taka ngumu kwenye mitaro kupitia  kaulimbiu  yake ya “Mitaro Sio Jalala”.

/ Published posts: 1209

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram