Na Mwandishi Wetu TANGA
Unamilikiwa na Watanzania kwa asilimia 100
Utafiti umebaini uwepo wa mashapo ya dhahabu kiasi cha tani 21.7
Kampuni ya PMM Tanzania Limited inayomiliki mgodi wa Magambazi imeanza shughuli za uzalishaji madini ya dhahabu ambapo kuanzia Agosti 2024 mgodi huo unatarajiwa kuzalisha kilo 25 za dhahabu kwa mwezi.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa PMM Tanzania Limited, Mhandisi Ulimbakisya Spendi baada ya timu ya Wanahabari kutoka Wizara ya Madini kutembelea eneo la mgodi huo uliopo wilaya ya Handeni mkoani Tanga.
Aidha, Spendi amesema mgodi huo upo katika milima ya Magambazi uligunduliwa na wachimbaji wadogo mnamo mwaka 2003 ambapo mwaka 2007 Kampuni ya Canaco iliomba leseni ya utafiti katika eneo hilo na mwaka 2009 iligundulika kwamba kuna dhahabu ambayo inaweza kuzalishwa kwa faida hivyo ikapelekea kuomba leseni ya uchimbaji wa Kati wa madini ya dhahabu.
Sambamba na hayo, Spendi amesema baada ya Serikali kuhamasisha uzalishaji katika mgodi huo, Canaco ililazimika kuuza leseni ya mgodi huo mwaka 2020 kwa Kampuni ya PMM ambayo inamilikiwa na Watanzania kwa asilimia 100.
Spendi amesema mgodi huo tayari umekwishafanyiwa utafiti na kubaini uwepo wa mashapo ya dhahabu kiasi cha tani 21.7 katika eneo hilo ambapo utafiti bado unaendelea katika mgodi huo.
Pia, Spendi amesema mpaka sasa mgodi huo umesaidia ukarabati wa Shule ya Msingi Magambazi, ujenzi wa vyoo katika shule hiyo na unaendelea na ujenzi wa Kituo cha Afya ambayo mpaka sasa imetumia kiasi cha shilingi milioni 400 ambapo mpaka kukamilika kwake inatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi milioni 700 ikiwa ni mchango wa mgodi huo kwa Jamii inayozunguka mgodi.
Pamoja na mambo mengine, Spendi amesema mgodi wa Magambazi una changamoto kubwa ya umeme ambapo Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limeahidi kwamba ifikapo mwezi Juni miundombinu ya umeme itakuwa imefika katika eneo la mgodi huo.