Na Mwandishi Wetu
Wananchi wa Kijiji cha Kwedikwazu kilichopo wilayani Handeni mkoa wa Tanga wameipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali zinazoendelea kufanyika ili kuleta maendeleo ya Kudumu kupitia Sekta ya Madini.
Hayo yamebainishwa na Katibu wa Kikundi cha Wanawake cha Mwanzo Mgumu, Bi Saumu Kisaka wakati akizungumza na timu ya Maafisa Habari wa Wizara ya Madini walipotembelea Mgodi wa Dolomite Mkoani humo.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wenzake, Kisaka amesema, Kikundi chao ambacho kina wanachama 12 kinajishughulisha na biashara ya kokoto za mapambo, ujenzi na uuzaji wa mawe mbalimbali yakiwemo mawe ya ujenzi, biashara inayowasaidia kujipatia kipato na kuendesha maisha yao ya kila siku.
Pamoja na mambo mengine, akizungumzia uzoefu wake, Kisaka amesema biashara ya uuzaji madini ya Dolomite (mawe meupe) inamsaidia kuendesha maisha yake ikiwemo kusomesha watoto, kujenga nyumba ya kuishi na kukidhi mahitaji ya lazima ikiwemo gharama za matibabu, mavazi na chakula.
Katika hatua nyingine, Kisaka ameiomba Serikali kusaidia upatikanaji wa masoko ya Madini hayo ya urembo na mashine ya usagaji wa mawe ambapo kwa sasa wanatumia nyundo za mkono kugonga mawe hayo ili kuongeza kipato kwa wananchi wanaoishi katika eneo la kijiji hicho na Tanzania kwa ujumla.
Pia, Kisaka ametumia nafasi hiyo kuishukuru timu ya Habari kutoka Wizara ya Madini kwa kutembelea eneo la uzalishaji na ufanyaji biashara ya madini hayo wilayani humo.
Awali, Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Tanga, Bi Winnifrida Mrema amesema shughuli za uchimbaji madini ya viwandani aina ya Dolomite katika kijiji cha Kwedikwazu zinafanywa na wachimbaji wadogo ambapo madini hayo husafirishwa kwenda kwenye viwanda katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Arusha kwa ajili ya kutengeneza wa rangi za majengo, mbolea, na viwanda vya kuchakataji kwaajili kutengeneza urembo wa majengo mbalimbali.
Aidha, Mrema amesema Mkoa wa Tanga umepata mafanikio makubwa kwa kuwepo machimbo hayo ambapo wananchi wa Kijiji hicho wamejipatia ajira ikiwemo kina mama wanaoponda na kuuza madini hayo kwa ajili ya urembo wa nyumbani na waendesha bodaboda wanaendelea kujipatia kipato kwa ubebaji wa madini hayo kutoka migodini mpaka katika eneo la barabara kwa ajili ya ufanyaji biashara pia wasafirishaji wa madini hayo kwa kutumia malori kutoka mgodini hapo mpaka viwandani.
Pamoja na mambo mengine, Mrema ametoa wito kwa Wawekezaji Wakubwa na Wadogo nchini kujitokeza na kuchukua Leseni za Uchimbaji wa Madini hayo kwa ajili ya kuleta tija na maendeleo kwa jamii.
Dolomite ni aina ya madini ya viwanda yanayotumika kwa ajili ya mapambo, ujenzi, utengenezaji wa rangi, pamoja na utengenezaji wa mbolea.