225 views 2 mins 0 comments

SERIKALI KUONGEZA BILIONI 4 KUKAMILISHA UPANUZI WA NJIA NNE BUKOBA MJINI

In KITAIFA
March 28, 2024



Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameeleza kuwa tayari Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia kuongeza kiasi cha Shilingi Bilioni 4 kukamilisha upanuzi wa barabara ya njia nne Bukoba Mjini (Rwamishenye Round about – Stendi ya Bukoba Mjini) yenye urefu kilometa 1.6.

Bashungwa amesema hayo leo tarehe 28 Machi 2024 wakati alipowasili katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Kagera kuanza ziara ya kikazi ya kukagua ujenzi wa miundombinu ya barabara Mkoani humo.

Bashungwa amesema kuwa awali Serikali ilitoa kiasi cha shilingi Bilioni 4.64 kuanza ujenzi wa wa barabara hiyo kwa kipande cha kilometa 1 ambacho kinaanzia Rwamishenye hadi eneo la Mitaga ambapo kwa sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 25.

Amesema kuwa kiasi cha shilingi Bilioni 4 kitakachoongezwa kitawezesha ujenzi wa kipande cha mita 600 kuanzia eneo la Mitaga hadi stendi na ujenzi wa daraja kubwa katika mto Kanoni.

โ€œMheshimiwa Rais ameshatoa kibali kwa TANROADS kuendeleza ujenzi wa barabara ya njia nne hadi stendi ya Bukoba ambapo Mkandarasi M/s Abemulo ambaye ameshaanza kazi kwa kipande cha km 1 ataendelea na ujenzi kwa kipande cha mita 600 na daraja kubwaโ€, amesema Bashungwa.

Aidha, Bashungwa amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Kagera kumsimamia Mkandarasi anayeendelea na ukarabarati wa barabara ya Lusahunga – Rusumo (km 92) kwa kiwango cha lami ambapo barabara hiyo inauunganisha Mkoa wa Kagera na nchi jirani.

Naye, Mbunge wa jimbo la Bukoba Mjini, Stephen Byabato amesema kazi ya ujenzi wa njia nne wa barabara ya Bukoba Mjini unaendelea kwa kasi kubwa na ameiomba Serikali kushughulikia suala la fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa barabara hiyo.

/ Published posts: 1215

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram