136 views 3 mins 0 comments

WIZRA YA UJENZI YAJIPANGA KUFANYA MATENGENEZO MIUNDOMBINU ILIYOATHIRIWA NA MVUA NA KUPUNGUZA FOLENI

In KITAIFA
March 25, 2024

Na mwandishi wetu

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2024/25 Wizara kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) itajikita katika kufanya matengenezo makubwa katika maeneo korofi yaliyoathiriwa na mvua pamoja na kuendelea kukamilisha utekelezaji wa miradi ya barabara na madaraja hususan ya kimkakati na ile ya kupunguza msongamano katika miji ya Dodoma, Mwanza, Mbeya, Arusha, Dar es Salaam na Morogoro.

Ameyasema hayo Machi 25, 2024 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu wakati Kamati ikipitisha vifungu vya Bajeti ya Fungu 98 ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2024/25 ambapo pamoja na mambo mengine  amesema kuwa mkakati uliopo ni kuhakikisha madaraja yote yaliyokatika yanarejeshwa katika hali yake.

“Nimshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametupatia kiasi cha Shilingi Bilioni 50 ambazo ni fedha za dharura kwa ajili ya matengenezo ya barabara zitakazosaidia kuboresha na kukarabati maeneo yote yalioathiriwa na mvua”, amesema Bashungwa.

Bashugwa ameeleza kuwa katika Jiji la Dodoma Wizara imepanga kupunguza msongamano wa magari kwa kukamilisha ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje wa Dodoma (km 112.3), kwa kiwango cha lami ifikapo mwezi Disemba, 2024 na kuanza upanuzi wa barabara kuanzia eneo la Mtumba hadi Roundabout ya Safina.

Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa mara baada ya usanifu kukamilika katika eneo la Mtanana Wizara imepanga kuboresha eneo hilo ambalo limekuwa likijaa maji kwa kupandisha tuta la barabara lenye urefu wa km 6 pamoja na kuweka makalvati makubwa yatakayoruhusu maji kupita kwa wingi bila athari yoyote.

Kadhalika, Bashungwa amesema kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari ameshatoa kibali cha kuanza utekelezaji wa miradi 29 ambayo ipo katika hatua za manununzi na utekelezaji wake unatarajiwa kuanza mwaka ujao wa fedha 2024/25.

Kuhusu suala la taa, Waziri Bashungwa amesema ameshatoa maelekezo kwa Mtendaji Mkuu wa TANROADS na tayari wameanza mchakato wa ununuzi wa taa kwa pamoja ili kuwa na viwango na ubora unaofanana pamoja na kupunguza gharama kwa taa zitakazofungwa katika miji na vijiji.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Selemani Kakoso (Mb), ameilekeza Wizara kuisaidia Wakala wa Majengo (TBA) na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kuhusu ukusanyaji wa madeni yao kwa Wizara na Taasisi wanazozidai ili fedha hizo ziwasaidie kutekeleza na kumaliza miradi waliopanga.

“Hakikisheni Wizara mnajielekeza kutafuta fedha,angalieni namna ya kuwa wabunifu kutafuta vyanzo vya upatikanaji wa fedha ili zisaidie kulipa madeni ya wakandarasi na kuwezesha miradi kuendelea”, amesema Kakoso.

/ Published posts: 1209

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram