621 views 3 mins 0 comments

TAMISEMI WATOA TAARIFA YA WAHITIMU YA KIDATO CHA NNE MWAKA 2023 MACHAGUO YA TAHASUSI ZA KIDATO CHA TANO

In KITAIFA
March 20, 2024

Na Madina Mohammed DAR ES SALAAM

Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za mitaa TAMISEMI wametoa taarifa kwa wahitimu wa Kidato cha Nne mwaka 2023 kuhusu fursa ya kubadilisha machaguo ya Tahasusi za Kidato cha Tano na Kozi za Vyuo vya Ualimu, Vyuo vya Kati na Elimu ya Ufundi kwenye mfumo wa kielektroniki wa uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga na Kidato cha Tano na Vyuo.

Ikiwa ni maandalizi ya awali ya uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga Kidato cha Tano na Vyuo vya Serikali Mwaka 2024.

Akizungumza na waandishi wa habari Leo Tarehe 18 Machi 2024 Jijini Dar es salaam Waziri wa Tamisemi Mohammed Mchengerwa Amesema Serikali imekuwa ikitoa fursa kwa wahitimu wa Kidato cha Nne kufanya mabadiliko ya machaguo ya Tahasusi (combination) na Kozi mbalimbali walizozichagua kupitia Fomu ya Uchaguzi (Selform.)

“Fursa hii huwawezesha wanafunzi kurekebisha machaguo yao kulingana na ufaulu waliopata kwenye matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA)”. Amesema Mchengerwa

Mchengerwa Amesema TAMISEMI imekamilisha zoezi la awali la kuingiza kwenye kanzidata taarifa zilizo kwenye Fomu za Uchaguzi za wanafunzi kama zilivyojazwa na wanafunzi wakiwa shuleni.

“Mabadiliko ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la Mwaka 2023 na Mitaala ya Elimu kwa Kidato cha Tano yameanza kutekelezwa, ambapo utekelezaji huo umehusisha uanzishaji wa Tahasusi mpya 49, kutoka 16 zilizokuwepo awali hadi kufikia tahasusi 65”. Ameongeza Mchengerwa

Tahasusi hizo mpya zitakazoanza kutekelezwa Julai, 2024 zipo katika makundi saba (7) ambayo ni: Tahasusi za Sayansi ya Jamii; Tahasusi za Lugha; Tahasusi za Masomo ya Biashara; Tahasusi za Sayansi; Tahasusi za Michezo; Tahasusi za Sanaa; na Tahasusi za Elimu ya Dini. Orodha ya masomo na Tahasusi zitakazoanza kutekelezwa Julai, 2024 (Rejeeni kiambatisho Na.1)

Mchengerwa Amesema Kukamilika kwa zoezi hili kunatoa fursa kwa wanafunzi kuweza kufanya mabadiliko ya machaguo/ tahasusi/ kozi kwa njia ya mtandao (online). Baada ya wanafunzi kufanya marekebisho yao, kanzidata hiyo ndiyo itakayotumika kuwachagua na kuwapangia nafasi za Kidato cha Tano na Kozi mbalimbali katika Vyuo vya Kati na vya Elimu ya Ufundi kwa kuzingatia sifa za ufaulu na machaguo yao.

Aidha Mchengerwa Amesema Zoezi la kubadilisha tahasusi na vyuo litaanza rasmi tarehe 19 Machi, 2024 hadi tarehe 30 Aprili, 2024. Wanafunzi, wazazi na walezi wanakumbushwa kushauriana kikamilifu ikiwa ni pamoja na kupata ushauri wa kitaalam na kitaaluma kabla ya kufanya mabadiliko ya tahasusi au Kozi.

/ Published posts: 1480

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram