Na mwandishi wetu
Walimu wa shule za Sekondari Vetenari, Temeke, Sandali na wanafunzi wa shule ya ya Temeke wamepewa elimu ya mbolea na kuombwa kuwa mabalozi wema kwenye jamii zao juu ya matumizi sahihi ya mbolea.
Elimu hiyo imetolewa na wawakilishi wa watumishi wanawake wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) ikiongozwa na Gema Nganyagwa Afisa Udhibiti Ubora ikiwa ni moja ya shughuli zinazotekelezwa kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani tarehe 8 machi, 2024.
Akizungumza wakati wa tukio hilo Diwani wa Kata ya Sandali Mhe. Christopher Mwansasu ameeleza kuwa, Tfra ni taasisi ambayo inayotambua na kushirikiana na jamii inayoizunguka katika hali zote.
Ameeleza kuwa, wamekuwa wakishirikiana sana katika shughuli mbalimbali za maendeleo na ndio maana wameona ni vyema kufika na kutoa elimu ya mbolea kwa wanafunzi wa shule hiyo iliyopo katika jamii yao.
“TFRA wanatambua kuwa elimu inaanzia chini na ndio maana wamechagua kundi hili ili kupanda mbegu inayowaandaa na kuwaonesha fursa zilizopo kwenye tasnia ya mbolea” amesema Diwani Mwansasu.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Temeke, Ingia Mtenga, ameishukuru TFRA kwa kuichagua shule anayoisimamia na kutoa elimu iliyowaongezea uelimu wa tasnia ya mboleaย wanafunzi na waalimu wao.
Amesema,ย shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 2767 miongoni mwao wanafunzi 501 ni wa kidato cha 5 na 6 huku ikiwa na jumla ya walimuย 60 na walimu 28 wakiwa ni wanawake.
Katika kuonesha uelewa walioupata kupitia elimu iliyotolewa wanafunzi waliulizwa maswali ikiwa ni pamoja na kutaka kujua tofauti kati ya mbolea za viwandani na samadi na kuhoji ni mbolea ipi inafaa zaidi
Aidha, walitaka kujua namna Mamlaka inavyowafikia wakulima wa vijijini kwa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea, kujua namna Serikali ilivyojipanga kutatua changamoto za upatikanaji wa mbolea za ruzuku uliojitokeza msimu wa kilimo 2022/2023 na changamoto ya kutokupatikana kwa baadhi ya mbolea pindi zinapohitajiwa na wakulima kwa kutolea mfano wa mbolea za Amidas.
Pia, wanafunzi hao walipenda kujua namna Mamlaka inavyodhibiti mbolea zinazozalishwa nchini lakini pia zile zinazoingizwa kutoka nje ya nchi na kupewa majibu Mujarabu kwa maswali yote yaliyoulizwa kutoka kwa wanawake hao.