Na mwandishi wetu
Katika kuelekea chaguzi za juu za Chama Cha ACT Wazalendo wagombea wa nafasi hizo wameshiriki kwenye mdahalo wa kunadi sera zao ulioandaliwa na chama hicho ukihusisha mgombea nafasi ya Mwenyekiti Othman Masoud Othman na nafasi ya Kiongozi wa Chama wagombea ni Dorothy Semu na Mbarara Maharagande.
Akizungumza katika mdahalo huo baada ya Mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti Juma Haji Duni kujitoa Mgombea Othman Masoud Othman ametaja mambo matatu ambayo atakifanyia Chama atakapoidhinishwa kushika nafasi hiyo.
Aidha ametaja mambo hayo kuwa ni Kukijenga chama na kujiendesha kama taasisi, Kukijenga chama katika utendaji na kuchukua uongozi wa nchi (dola).
Othman ambaye kwa sasa ni Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Zanzibar akifafanua kuhusu kukijenga chama kitaasisi, amesema pamoja na kwamba Chama bado kichanga lakini kimefanya mambo makubwa na kina fursa ya kujijenga kisasa.
“Hivyo tunahitaji kukijienga chama kama taasisi katika ngazi zote, kujenga misingi ya uongozi, hivyo ni lazima tujijenge kitaaisi, twende kwa mujibu wa taratibu kama taasisi,” amesema Othman.
Makamu huyo wa Kwanza wa Rais wa Zanziba akieleza kwa upande wa kukijenga chama kiutendaji, ameeleza kuwa atahakikisha chama kinawafikia wananchi, wanawafahamisha na kuwaeleza walipofikia kama chama.
Kuhusu kuhakikisha ACT Wazalendo wanashika uongozi wa nchi (Dola) Othman amesema atahakikisha wanashirikiana na vyama vyote vya siasa pamoja na wadau wote.
“Tatizo tulilonalo kila Chama kina Tanzania yake, hivyo nchi haiwezi kwenda hivyo. Sisi kama ACT Wazalendo tunayo fursa ya kuonesha mfano na njia. Tunavyoamini ni kwamba tufike mahali tuwe na maono ya namna gani tunataka kuiendesha Tanzania,” ameongeza Othman.
Mdahalo huo ulihudhuriwa na Wanachama wa Chama Cha ACT Wazalendo kwa kuwauliza maswali wagombea na kupata ufafanuzi wa kile ambacho watakifanya katika kukipeleka mbele chama hicho.