MHADHIRI Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dkt. Azaveli Lwaitama amesema kazi ya Wazee wa Chama cha ACT Wazalendo ni kuwa washauri wa chama hususan kwa vijana ili kuwa katika njia sahihi ya ujenzi wa umoja kwa maslahi ya Taifa.
Dkt. Lwaitama amesema hayo leo Machi 1, 2024 akihutubia katika Mkutano Mkuu wa Ngome ya Wazee wa Chama cha ACT Wazalendo uliofanyika katika ukumbi wa Hakainde Hechilema Makao Makuu ya Chama yaliyopo Magomeni jijini Dar es Salaam.
“Wazee wa ACT Wazalendo kazi yenu kushauri vijana moto moto, wenye mihemko, kwani vijana pomoja na kushindana kwa hoja wanatakiwa kuhakikisha wanazingatia kulinda umoja kwani kazi kuu ya vyama hivi vya upinzani ni kuhakikisha wanakiondoa Chama cha Mapinduzi (CCM) madarakani na sio kushindana kwa kutukanana na kukashifiana,” amesema Dkt. Lwaitama.
Dkt. Lwaitama ameeleza kuwa vijana wamekuwa na kawaida ya kufanya mambo pasipo kutafakari matokeo ya maabaye, hivyo amewasisitiza Wazee wa ACT Wazalendo kuhakikisha vijana kabala hawajafanya jambo wewe na tabia ya kufanya tafakuri.
“Vijana wana kawaida ya kusema tutende kwanza mambo mengine yatajulikana baadaye, lakini kama Wazee mnatakiwa kuwaambia wasubiri kwanza, hekima, busara na maarifa yenu yanahitajika sana kwa mustakabali wa mienendo ya vijana ndani ya vyama,” amesisitiza Dkt. Lwaitama.
Hivyo ametumia fursa hiyo kuvitaka vyama vya upanzani kuheshimiana na kwamba Taifa litafika mbali kama vyama vitaingia madarakani kwa kuchaguliwa katika uchaguzi wa huru na haki unaofuata misingi ya Demokrasia.
Kwa upande wake Mshauri wa Chama hicho Juma Saanani akizungumza katika Mkutano huo uliokwenda sambamba na uchaguzi wa Viongozi wa Ngome ya Wazee ACT Wazalendo Taifa ametoa rai kwamba baada ya uchaguzi wabaki wamoja.
“Nawaomba Wazee wenzangu, tutachagua mmoja, tubaki pamoja na tutakuwa sote ni washindi,” amesema Saanani.