150 views 3 mins 0 comments

BARABARA YA TANGA-KILOSA-MIKUMI-LUPEMBE KUPANDISHWA HADHI KUWA BARABARA KUU ‘TRUNK ROAD’

In KITAIFA
February 23, 2024

MOROGORO

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Mhandisi Aisha Amour kuipandisha hadhi barabara ya Tanga – Kilosa – Mikumi – Lupembe – Njombe kuwa barabara kuu ‘Trunk Road’ ili kuinua uchumi katika mikoa yaTanga, Morogoro na Njombe ambapo barabara hiyo inapita.

Bashungwa, ameyasema hayo wakati anakagua Ujenzi wa Barabara ya Dumila-Kilosa-Ulaya-Mikumi (km 142) kwa kiwango cha lami sehemu ya Rudewa-Kilosa (Km 24) Mkoani Morogoro ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 98.

“Barabara inayoanzia Tanga bandarini kupitia Handeni – Mziha – Dumira – Kilosa – Mikumi – Ifakara mpaka Lupembe Njombe lazima tuitangaze iwe Trunk road ili kuipatia bajeti ya kutosha kuweza kuihudumia maana tukiipandisha hadhi tutaweza kuihudumia kwa uzito kwa sabau ni barabara inayoungasha nchi kutoka mpaka mmoja hadi mwingine” amesema Bashungwa



Bashungwa akijibu ombi la Mbunge wa kilosa, Prof. Palamagamba Kabudi la uwekaji wa taa, amesma Wizara itatenga bajeti ya ufungaji wa taa 120 katika kipande cha kilometa 3 katika barabara ya Rudewa – Kilosa.

Aidha,  Waziri Bashungwa amemuelekeza Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Morogoro kuhakikisha wanatenga bajeti za matengenezo ya upanuzi wa njia ya maji katika mito yote ili mvua zitakaponyesha zisilete athari katika maeneo hayo na maeneo jirani.



Amemtaka Mkandarasi M/s Umoja Kilosa JV kujenga barabara na Madaraja usiku na mchana na kuhakikisha inakamilika kwa wakati kama ilivyopangwa kwenye mkataba kwani fedha zote zimeshalipwa na ifakapo mwezi wa nne mwishoni wataikabidhi Barabara hiyo kwa wananchi.

Akitoa taarifa ya mradi kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini  (TANROADS), Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi wa miradi, Mhandisi Malima Kusesa, amesema mradi wa ujenzi wa barabara ya Dumila-Kilosa-Ulaya-Mikumi (km 142) kwa kiwango cha lami sehemu ya pili, Rudewa-Kilosa (Km 24) umefikia asilimia 98.3 na sehemu iliyobaki ni ujenzi wa madaraja matatu ambayo yanaunganisha barabara hiyo.



Vilevile ameongeza kwa kusema kuwa Mradi huo unafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 100.

Kwa upande wake Mbunge wa Kilosa, Profesa Palamagamba Kabudi, ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita chini ya Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza ujenzi wa barabara ya Dumila-Kilosa, kipande cha kutoka Rudewa-Kilosa (km 24) kwa kiwango cha lami.

Kukamilika kwa mradi huu kutakuza uchumi kwa kuwa mradi huu ni kiunganishi cha mikoa ya kaskazini ( Tanga, Kilimanjaro na Arusha) na Mikoa ya Kusini (Iringa, Mbeya na Ruvuma) kupitia Turiani na Mziha.

/ Published posts: 1209

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram