146 views 3 mins 0 comments

SERIKALI YAISHUKURU BENKI YA DUNIA KUFANIKISHA MRADI WA DMDP

In BIASHARA, KITAIFA
February 20, 2024

Waziri wa Nchi,Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP) awamu ya pili utajenga barabara za lami katika Mkoa wa Dar es salaam kilomita 250, kuanzisha mfumo wa udhibiti wa taka ngumu, masoko 18 pamoja na vituo vya mabasi tisa.

Mhe.Mchengerwa ameyasema hayo leo Februari 20, 2024 jijini Dar es salaam kwenye hafla ya utiaji saini mkataba wa fedha za mradi huo  kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki ya Dunia ambapo waliotia saini ni Waziri wa Fedha na Mpango, Mhe. Dkt.mwigulu nchemba na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Nathan Belete.

Akizungumza baada ya kusainiwa mikataba hiyo,
Waziri Mchengerwa amesema Jiji hilo limekuwa na changamoto ya miundombinu, ikiwamo ya barabara, ambapo awamu ya kwanza ya DMDP iliboresha jumla ya kilometa 207 katika Halmashauri tatu zilizokuwa chini ya mradi na imeleta  mabadiliko makubwa.



“Sasa hivi mradi huu utatekelezwa  kwenye halmashauri zote za mkoa wa Dar es salaam kila halmashauri itajengewa barabara za lami,  masoko pamoja na vituo vya mabasi, mradi unaenda kuangalia changamoto ya usimamizi wa taka ngumu katika Jiji la Dar es Salaam kwa ujumla wake.”

“Kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi juu ya taka kutochukuliwa kwa wakati na vilevile makandarasi wa kukusanya taka ngumu kuwa na mazingira ambayo sio rafiki kwa kufanya majukumu yao kwa ufanisi,mradi huu unatarajiwa kuboresha miundombinu ya taka ngumu kwa maana ya kuanzia katika ukusanyaji, usafirishaji hadi utunzaji wake katika madampo ya kisasa matatu yanatarajiwa kujengwa chini ya mradi huu,” amesema
Mchengerwa.



Kadhalika, amesema kupitia mradi  huo master plan ya mifereji mikubwa ya maji ya mvua itaboreshwa na mifereji muhimu itatambuliwa na itajengewa yenye jumla ya kilometa 90 kwa Dar es Salaam nzima.

“Mradi huu ni ishara kuwa Serikali ina nia thabiti ya kutatua changamoto za miundombinu ya Dar es Salaam na kubadilisha hali ya Jiji letu,” amesisitiza Mchengerwa.


Naye, Waziri wa Fedha Mhe.mwigulu nchemba amesema  mradi huo utatakelezwa kwa muda wa miaka sita kuanzia mwaka 2024/25 na gharama yake ni EURO milioni 361.1 sawa na sh. bilioni 988.083 zitaleta mabadiliko chanya makubwa katika Jiji  la Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkaazi wa WBTanzania , Nathan Belete amesema ni fahari kwao kushiriki katika kukuza na kuendeleza Jiji la Dar es salaam, kwa zaidi ya miaka 15 iliyopita Benki ya Dunia imetoa zaidi ya Dola bilioni  1.5 kwa ajili ya uendelezaji wa Jiji la Dar es salaam.



Benki ya Dunia kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI wamekwishatoa fedha nyingi kwa ajili ya kutatua changamoto za miji ya Tanzania hasa katika kuboresha miundombinu muhimu ya mijini ikiwamo mradi wa ULGSP, TSCP pamoja na DMDP awamu ya kwanza na kwa sasa  wametoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa  mradi wa TACTIC katika miji 45 nchini.

/ Published posts: 1209

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram