Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA Mabula Misungwi Nyanda amewataka Maofisa wote wa taasisi hiyo kuweka mikakati madhubuti ya kuongeza idadi ya watalii ili kuongeza mapato Serikalini ikiwa ni pamoja na kuboresha ulinzi na usimamizi wa rasilimali za wanyamapori na malikale.
Kamishna Mabula ameyasema hayo leo Februari 10, 2024 alipokuwa akiongea na Maofisa wa taasisi hiyo katika kikao kazi cha maandalizi ya bajeti kwa Mwaka wa fedha 2024/2025 kinachofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo Mkoani Iringa.
“Tumeaminiwa na Serikali kusimamia rasilimali hizi kwa niaba ya wananchi, hivyo hakikisheni mnaibua vyanzo vipya na fursa za mapato ili kuongeza mchango wa Mamlaka katika mfuko Mkuu wa Serikali na kuboresha ulinzi na usimamizi wa rasilimali za wanyamapori na malikale” amesema
Aidha Kamishna huyo amesema katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita TAWA katika kutekeleza jukumu lake la msingi la kuhifadhi, kusimamia na kuendeleza Rasilimali ya Wanyamapori na Malikale ilifanikiwa kupunguza ujangili wa tembo ikiwa ni pamoja na kudhibiti madhara ya matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu
Amesema katika kipindi cha mwaka 2022/23 pekee kulikuwa na matukio 2, 817 ambapo jumla ya *”Doria Siku watu” 18,894* za usiku na mchana zilifanyika ili kuhakikisha maisha na mali za wananchi vinakuwa salama.
Sanjari na hilo Kamishna Mabula amewataka Maofisa hao kudumisha mahusiano na ushirikiano baina yao na KUU za Wilaya na Mikoa pamoja na kutumia Askari wa Vijiji (VGS) katika kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu.
Pia Mabula amesema TAWA ilifanikiwa kutatua migogoro ya mipaka kwa kukamilisha usimikaji wa vigingi katika mapori ya akiba Swagaswaga, Mkungunero, Selous, Liparamba, Mpanga/Kipengere, Wamimbiki na Igombe na kazi ya kuweka vigingi katika Pori la Akiba Kilombero inaendelea na ipo katika hatua nzuri.
Katika hatua nyingine Kamishna Mabula amesema katika Mwaka wa Fedha 2024/25 TAWA imejiwekea vipaumbele vya mpango na bajeti ambavyo vinalenga kuongeza ufanisi na tija katika utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo
Akibainisha vipaumbele hivyo Mabula amesema ulinzi na usimamizi wa Rasilimali za Wanyamapori na Malikale pamoja na kuimarisha utalii na kuongeza mapato ni vipaumbele mahsusi katika Mwaka ujao wa fedha
Vingine ni utatuzi wa migogoro ya mipaka na udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu pamoja na kuimarisha mazingira ya utendaji kazi kwa watumishi na uwezo wa taasisi kutoa huduma.
Kwa upande wake
Kamanda wa Uhifadhi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Kamishna Msaidizi Mwandamizi Sylvester S. Mushi amemuhakikishia Kamishna Mabula kuwa Maofisa hao watafanya Kila wawezalo kuhakikisha wanaongeza ubunifu na usimamizi wa mapato