214 views 2 mins 0 comments

MELI KUBWA YA NORWEGIAN DAWN IMEINGIA DAR ES SALAAM IKIWA NA WATALII 2,210

In KITAIFA
January 16, 2024

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania, Damasi Mfugale amesema kuwa utalii wa meli ambao kwa sasa ni zao la kimkakati nchini unakwenda kukua kwa kiasi kikubwa kadri siku zinavyokwenda ambapo idadi ya watalii itaendelea kuongeza.

Mfugale ameyasema hayo leo Januari 16, 2024 wakati wa mapokezi ya meli kubwa iliyotia nanga katika bandari ya Dar es Salaam ikiwa na jumla ya watalii 2,200 kutoka mataifa mbalimbali duniani inayozunguka kwa ajili ya kufanya utalii ambapo kwa Tanzania ilianzia visiwani Zanzibar.

“Kwa niaba ya bodi pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii tunayo furaha kubwa kupokea meli hii kubwa ya Norwegian Dawn, imefika leo saa 12 asubuhi ikiwa imechukua watalii takribani elfu mbili na mia mbili. Watalii hawa ambao zao letu la kimkakati sekta yetu ya utalii wanafahamika kama ni Watalii wa Meli au Cruise Ship Tour isim, tunategemea katika kipindi cha miaka miwili au mmoja kuongeza idadi ya meli hizi kuja Tanzania”, amesema Mfugale.

Aidha Mkurugenzi huyo amesema kuwa katika suala ya uchumi mpana wa utalii maana yake ni kwamba wageni wakija Tanzania watatembelea sehemu mbalimbali. “ Kwa mfano hawa wataondoka leo kwenda Selous, wengine wataenda maeneo mbalimbali hapa Dar es Salaam , wengine Museum na wengine wanakwenda Bagamoyo.

“Kila wanapokwenda huko watatumia kama kwenye migahawa, kama ni kulipa kiingilio kwenye sehemu mbalimbali za vivutio. Kwa hiyo tunajivunia na hizi zote ni jitihada za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na tunategemea meli hizi zitaendelea kuja na mwezi ujao wa pili tutakuwa na meli nyingine kubwa itakayokuja, hiyo ni katika muendelezo wa kuhakikisha kwamba utalii wa meli unakua,” amesema Mfugale.

/ Published posts: 1209

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram