277 views 3 mins 0 comments

TATO NA BONITE ZAUNGANA NA SERIKALI KWA KUTOA MISAADA KWA WAATHIRIKA WA MAAFA.HANANG

In KITAIFA
December 07, 2023

SERIKALI imeendelea kupokea misaada mbalimbali ya kibinadamu kwa ajili ya kusaidia waathirika wa maafa ya mafuriko na maporomoko ya mawe na tope kutoka mlima Hanang’ mkoani Manyara.

Akipokea misaada hiyo kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama hii leo Disemba 07, 2023 Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki amezishukuru taasisi hizo mbili za TATO(Tanzania Association of Tour Operators) na Bonite Bottlers Ltd. kwa kuungana na Serikali katika kusaidia waathirika wa maafa yaliyotokea tarehe 03 Disemba 2023 mkoani humo huku akiwasihi wadau kuendelea kujitokeza kuchangia kwa hali na mali ili kuendelea kurejesha hali kwa wananchi hao.

“Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu nimepokea misaada hii na tunawashukuru sana kwa namna mlivyoungana na Serikali, nichukue nafasi hii kuwaomba wadau wengine kuendelea kuungana na Watanzania wenzetu ili kuona namna tunavyoweza kuwasaidia,” alisema Mhe. Kairuki.

Aidha, alitumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wadau kujitokeza kwa kuzingatia ukubwa wa mahitaji uliopo ikiwemo vifaa vya ujenzi ili kutoa unafuu kwa waathirika wa tukio hilo.

Akizungumza mara baada ya kupokea vifaa hivyo Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi ametoa shukrani kwa misaada hiyo huku akieleza kuwa maji yaliyokabidhiwa yatasaidia kuendelea kujilinda na magonjwa ya milipuko kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama kwa afya zao.

“Asanteni sana kampuni ya BONITE pamoja na TATO kwa kuona umuhimu wa kutukimbilia, na mmetoa misaada itayosaidia ndugu zetu waliopata maafa haya na hii inatupa nguvu katika kurejesha hali huku tukiendelea kuungana pamoja kwa lengo moja la kuwasaidia,” alisema.

Naye, Bw. Wilbord Chambulo ambaye ni Mwenyekiti wa TATO Arusha (Tanzania Association of Tour Operators) akieleza misaada waliyokabidhi ikiwemo unga wa ngano tani kumi, maji ya kunywa lita 37,800 na mafuta ya kula lita 2000.

“Tumekabidhi na tutaendelea kujitoa ila chama kimeona umuhimu wa kuungana na Watanzania wenzetu kwa tukio hili zito la maafa, sisi TATO tutaendelea kufanya hivyo kwa kuzingatia ni ndugu zetu na maafa haya yametokea kama jambo la dharura hawakulitarajia,”alisema.

Kwa upande wake Meneja wa Mauzo Kampuni ya BONITE Mkoa wa Manyara, Bw. Thadeus Massawe ameeleza kuwa, wamekabidhi msaada wa maji ya kunywa aina ya Kilimanjaro katoni 1000 ikiwa ni sehemu ya misaada watakayoendelea kutoa kwa waathirika wa maafa hayo.

“Tumekabidhi msaada huu leo ikiwa ni sehemu tu, tutaendelea kutoa misaada zaidi kwa ndugu zetu na Kampuni inawapa pole waathiriwa wote wa maafa haya,” alieleza Massawe.

/ Published posts: 1214

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram