191 views 2 mins 0 comments

TAWA YAMWAGA MABILIONI BABATI SHUGHULI ZA UTALII ZANEEMESHA WANANCHI

In KITAIFA
November 16, 2023

SERIKALI kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) katika kipindi cha mwaka 2022/23 imetoa zaidi ya Billioni Mbili kwa Halmashauri ya wilaya ya Babati na Jumuhiya ya Uhifadhi ya Wanyamapori Burunge (JUHIBU) ikiwa ni kurejesha kwa jamii faida zitokanazo na shughuli za utalii zinazofanywa na TAWA wilayani humo.

Hayo yamesemwa Novemba 15, 2023 na Mkuu wa Wilaya ya Babati Mhe. Lazaro Twange wakati wa ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo itokanayo na gawio linalopatikana kutokana na shughuli za uwindaji wa kitalii na utalii wa picha iliyofanywa na TAWA Mkoani Manyara

“Pato linalopatikana kutokana na shughuli za uhifadhi pamoja na makato mengine yanayosambaa maeneo mengi, kiwango kikubwa sana kinarudi kwa wananchi” amesema

“Kwa mfano siku za hivi karibuni hii Jumuhiya ya hifadhi ya Wanyamapori Burunge iliyopo hapa kwangu Babati wamepata zaidi ya Shillingi Bilioni mbili ambazo zimegawanywa katika vijiji vyote kumi” ameongeza

Mhe. Lazaro amesema kutokana na fedha hizo zipo Zahanati zimejengwa mpaka zimetimia na kuwekewa vifaa tiba pia miradi mingine kama nyumba za waganga, mabweni katika shule ya Sekondari Mbugwe na miradi mingine mingi

Aidha, Mkuu huyo wa wilaya ameipongeza TAWA kwa kazi kubwa inayofanya wilayani humo kiasi cha kupelekea ujangili kupungua kwasababu wananchi wanaona manufaa ya moja kwa moja yanayotokana na shughuli za uhifadhi na utalii

Naye Mkurugenzi wa H/W ya Babati Anna Mbogo amesema kupitia mapato ya utalii wa picha na uwindaji wa kitalii asilimia kumi ya mapato hayo huwa inarudi katika ngazi ya Halmashauri na asilimia 65 inapelekwa katika Jumuhiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Burunge ambayo ina jumla ya vijiji kumi na asilimia 25 kubaki TAWA, ambapo fedha hizo hutumika katika miradi mbalimbali ya maendeleo kwa manufaa ya jamii

Akifafanua mgawanyo wa fedha hizo, Afisa Habari wa TAWA Beatus Maganja amesema katika kipindi cha Mwaka 2022/23 Halmashauri ya wilaya ya Babati ilipata zaidi ya Millioni Mia tatu na Jumuhiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Burunge zaidi ya Bilioni Mbili fedha ambazo zimetokana na shughuli za utalii.

Aidha amewaomba wananchi kushirikiana na Mamlaka hiyo katika ulinzi wa rasilimali za Wanyamapori ikiwemo kulinda na kutunza mazingira kwani pasipo uhifadhi imara shughuli za utalii zitazorota na hivyo kulikosesha Taifa pato ambalo lingeweza kuongeza miradi mingi ya maendeleo katika jamii mbalimbali nchini.

/ Published posts: 1214

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram