216 views 2 mins 0 comments

RC CHALAMILA BEHEWA KWA BEHEWA KUSIKILIZA KERO USAFIRI WA TRENI KAMATA -PUGU

In KITAIFA
November 09, 2023

Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Mhe Albert Chalamila akiwa ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe Edward Mpogolo leo Novemba 8,2023 amefanya ziara kwa treni za mjini kutoka stesheni ya Kamata kwenda Pugu kuona adha wanazokumbana nazo abiria. 

Mhe Albert Chalamila alitumia usafiri huo ili kuweza kuwasikiliza abiria na kuona kero na changamoto wanazokumbana nazo abiria na aliwaeleza kuwa mhe Rais Dkt Samia S. Hassan amewaona jinsi walivyodandia na kuning’inia kwenye treni hivyo amemuagiza afuatilie kujua ukweli wa Changamoto hiyo.

Aidha Abiria waliokua wakitumia usafiri huo walitumia fursa hiyo kumwelezea RC kero zao zikiwemo matumizi mabaya ya tiketi na ukataji wake, kutokuwepo usimamizi mzuri kwenye mabehewa ya wanafunzi na wazee, kuboreshwa huduma za vyoo, kukosa vituo vya kujikinga na mvua au jua,  na wengine waliomba kuongezewa siku ya jumamosi wapate huduma za treni sababu pilikapilika bado nyingi na pia kuboreshwe geti la kutokea pale Kamata.

Hata hivyo RC Chalamila alisema changamoto hizo kwa sehemu kubwa zitatatuliwa hivyo ameaidi kuendelea kuzitatua na pia kufanya ziara za kushtukiza na za taarifa ili kuwasaidia wananchi. 

Pia Mhe Chalamila amemtaka mkandarasi anayejenga barabara ya Pugu ajenge barabara za kando kuepuka wananchi kukwama kwenye foleni na kusababisha watu kuchelewa kazini, “Kipande cha kutoka Banana mpaka mitaa ya Ukonga, magari mengi yanapita kwenye njia moja kwahiyo tumekubaliana mchina aongeze barabara ili magari yaweze kupishana,” alisema.

Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Amina Lumuli aliwaahidi abiria wanaendelea kutatua changamoto wanazopata  na hadi sasa washaongeza ‘ruti’ na kufikia 8 hivyo abiria watasafiri kwa wakati na salama kufika kwenye shughuli zao au makwao, na alitoa wito kwa wananchi wote wafuate sheria na taratibu usafiri huo.

/ Published posts: 1480

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram