
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko leo Novemba 06, 2023 ameongoza Viongozi mbalimbali wa Serikali katika mazishi ya Mzee Issa Nangalapa ambaye ni kaka wa Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Wilaya ya Ruangwa, Lindi.
Akizungumza katika ibada ya mazishi Dkt. Biteko amempa pole Mheshimiwa Majaliwa na kwamba ujio wa viongozi katika msiba huo ni ishara ya upendo walio nao kwake.
“Sisi ni kielelezo kuwa Watanzania wanaupendo nawe ndio maana tumekuja kuungana pamoja na wewe, kulia pamoja na wewe lakini kukutia moyo kwamba sisi tuliofika hapa na wengine tunakupa pole kwa msiba wa kumpoteza kaka,” ameeleza Dkt. Biteko.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa amewashukuru Watanzania kwa kumfariji katika kipindi hichi cha msiba wa kaka yake. Amesema amepokea salamu za pole kutoka kwa Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar, Dkt.Hussein Mwinyi na watanzania wote wanaompa pole na kumfariji.