155 views 3 mins 0 comments

WAZIRI MKUU AZINDUA MASHINE YA KUCHANGANYA VIRUTUBISHO

In KITAIFA
October 26, 2023

Waziri mkuu Kassim Majaliwa amezindua mashine ya kuchanganya virutubisho kwenye vyakula na kuwaomba wadau wote wa maendeleo kuunga mkono juhudi hizo ili kuwezesha mashine hizo kuzalishwa kwa wingi kutumika katika maeneo yote hapa nchini.

Mashine iliyozinduliwa inatumika kuongeza virutubisho muhimu katika vyakula hususan unga wa mahindi, virutubisho hivyo ni pamoja na vitamin B na folic acid ambayo zinasaidia kwenye ukuaji wa watoto na kuzia kuzaliwa na changamoto za ulemavu ikiwemo mgongo wazi na vichwa vikubwa.

Waziri Mkuu amezindua mashine hiyo leo (Alhamisi, Oktoba 26, 2023) wakati akitembelea mabanda ya maonesho kabla ya kufunga Mkutano Mkuu wa Tisa wa Wadau wa Lishe nchini uliofanyika katika Hoteli ya Mount Meru Jijini Arusha. “Ninawapongeza sana wote waliowezesha kufikia hatua hii sambamba na mchango wa Shirika la GAIN, SIDO na DIT kwa kuwezesha kazi hii kukamilika.”

Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwasisitiza wadau hao wahakikishe virutubisho vinavyotumika katika mashine hizo vinazalishwa nchini ili kuondokana na utegemezi wa kuviagiza kutoka nje ya nchi.

Aidha, Waziri Mkuu amewahakikishia wadau hao kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan siku zote itaendelea kuunga mkono juhudi hizi ili kuhakikisha zinakuwa endelevu. Kadhalika,

Waziri Mkuu amesisitza Ofisi ya Rais – TAMISEMI ihakikishe kuwa mikataba ya lishe kati ya Mheshimiwa Rais na Wakuu wa Mikoa inatekelezwa kikamilifu na kuwa na tija. “Fanyeni ufuatiliaji wa karibu na kutoa taarifa za utekelezaji mara kwa mara.”

“Watendaji Wakuu wote wa Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala na Taasisi za Umma na Binafsi pamoja na Wadau wa Maendeleo na Asasi za Kijamii wekeni malengo ya lishe katika mipango yenu pamoja na kutenga fedha za utekelezaji kila mwaka kwa mujibu wa viwango tulivyojiwekea.”

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama amesema kwa kipindi kirefu nchi imekuwa ikikabiliana na changamoto ya upatikanaji wa vifaa vya kuchanganyia virutubisho kwenye vyakula vyenye bei nafuu, hivyo ameishukuru shirika la GAIN kwa kuwezesha upatikanaji wa vifaa hivyo.

“Serikali imepata mafanikio makubwa hayo kupitia Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) na Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na Shirika la GAIN ambalo limewezesha kukamilika kwa kazi hiyo na kuwa wa kwanza kununua na kusambaza mashine hizo katika maeneo tofauti 50 yenye wazalishaji wadogo ambao ndio kundi kubwa linalolisha wananchi wengi.”

Awali, Naibu Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI, Deogratius Ndejembi alisema TAMISEMI itaendelea kusimamia utekelezaji wa huduma za afua za lishe kwa wakuu wa mikoa pamoja na viongozi wa Mamlaka za Seikali za Mitaa kama ilivyoainishwa katika mikataba.

Lengo kuu la Mkutano huo ni kupokea tathmini ya utekelezaji wa masuala ya lishe nchini kwa mwaka uliopita na kutoa fursa nyingine kwa wadau wa lishe kukutana na kupata maelezo ya tathmini ya utekelezaji wa masuala ya lishe katika mwaka wa pili wa utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Pili wa Kitaifa wa Lishe (2021/22 – 2025/26) ambao ulizinduliwa mwaka 2021 Mkoani Tanga.

/ Published posts: 1480

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram