TAFIRI watakiwa kuwa kimbilio la wavuvi
Asisitiza utunzaji wa mazingira kupewa kipaumbele
Ahimiza kuongeza kasi kuuza bidhaa nje ya nchi
Dkt. Biteko Azindua ‘App’ kusaidia Sekta ya Uvuvi
Dar es Salaam
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewaagiza watendaji wa Sekta ya Uvuvi nchini kuifanya Sekta hiyo kuwa nyenzo muhimu ya kuondoa umaskini nchini.
Amesema, lengo ni kuiwezesha Sekta ya Uvuvi iwe na mchango mkubwa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Dkt. Biteko ameyasema hayo leo Oktoba 26, 2023 wakati wa Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 40 ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) sambamba na kuzindua mfumo maalum wa upatikanaji wa taarifa sahihi za uvuvi na kushuhudia utiaji saini wa makubaliano ya TAFIRI na ZAFIRI kwenye mazao ya bahari iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
“Hakikisheni kuwa, Wizara pamoja na TAFIRI mnakuwa kimbilio la wavuvi wakiwaona ninyi wajue majibu ya maswali yao watayapata kwenu, na muone fahari ya kuwaona wavuvi wanakuwa matajiri,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Aidha, Dkt. Biteko ameitaka TAFIRI kuongeza mchango wa mauzo ya bidhaa nje ya nchi ili kuweza kuleta fedha zaidi za kigeni ambayo imekuwa changamoto kubwa kwenye uchumi wa nchi. Amesema kuwa, “Mauzo ya bidhaa yameongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 168 mwaka uliopita hadi kufikia Dola za Marekani milioni 249,” ameeleza Dkt. Biteko.
Vile vile, amewataka TAFIRI kuwa mabalozi wa uhifadhi wa mazingira, vyanzo vya maji akisisitiza vilindwe kwa sababu Sekta hiyo inategemea vyanzo vya maji ili nchi iweze kujengwa kwa kulinda rasilimali hizo muhimu nchini.
Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema kuwa, wizara imehakikisha Sekta ya Uvuvi inakuwa na mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa na amesisitiza kuwa Sekta hiyo inaweka mazingira mazuri ili kuvutia uwekezaji na wavuvi wanufaike na rasilimali hiyo.
Katika hatua nyingine, Mhe. Ulega amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha takriban shilingi bilioni 25 kwa ajili ya kusaidia Sekta ya Uvuvi nchini
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TAFIRI, Dkt Ismael Kimirei amesema kuwa taasisi yake kupitia mfumo huo mpya wa upatikanaji wa taarifa kwa wavuvi utawasaidia wavuvi kujua makundi ya samaki yaliyopo kupitia simu zao na kuachana na uvuvi wa kubahatisha. Ameongeza kuwa, taasisi hiyo ni muhimili muhimu katika Sekta ya Uvuvi.