138 views 3 mins 0 comments

SH,BILIONI 163 KUTUMIKA KUIUNGANISHA KATAVI KATIKA GRIDI YA TAIFA

In KITAIFA
October 08, 2023

Kapinga aonya watakaokwamisha mradi

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe.Judith Kapinga amesema kuwa, shilingi Bilioni 163 zitatumika kuunganisha Mkoa wa Katavi katika Gridi ya Taifa na hivyo kuwezesha mkoa huo kupata umeme wa uhakika na unaotabirika.

Mhe. Kapinga amesema hayo wakati akizungumza na Wananchi wa Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi wakati wa ziara Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo mkoani humo tarehe 7 Oktoba 2023.

Kapinga amesema kuwa, mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Juni mwaka 2024 na kutoa onyo kuwa, watakaosababisha mradi huo kutokukamilika kwa wakati uliopangwa watachukuliwa hatua.

“Wizara ya Nishati haitakuwa na kikwazo kuhakikisha Katavi inapata umeme mwingi na wa uhakika kwa kuwa tayari tumejipanga na fedha zipo, yeyote akayeshindwa kutekeleza mradi huo kwa wakati, ufanisi na weledi kama ilivyoelekezwa atachukuliwa hatua kali za kisheria,”alisema Mhe. Kapinga.

Ameeleza kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha hizo ili kuhakikisha kuwa Mkoa wa Katavi unapata umeme wa uhakika na kuondokana na umeme unaozalishwa kwa kutumia mafuta kwani una gharama kubwa.


Amesema fedha hizo zitatumika katika kujenga mradi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka mkoani Tabora hadi Katavi pamoja na vituo vitatu kupoza na kusambaza umeme vya Ipole, Inyonga na Uhuru ambapo Kituo cha Uhuru kilichopo wilayani Urambo mkoani Tabora ujenzi wake unaendelea vizuri na umefikia asilimia 60 ya utekelezaji wake.

Kuhusu njia ya kusafirisha umeme amesema ujenzi wake umefikia 40%, na kwamba vifaa vyote vinavyohitajika katika eneo la mradi vitakuwa vimefika katika maeneo ya kazi ifikapo mwishoni mwa mwezi Oktoba, ili mwezi Juni 2024, umeme wa gridi uwe umefika Katavi.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri amekagua ujenzi wa Kituo cha Kupoza na Kusambaza umeme cha Mpanda kinachojengwa na Kampuni ya Tanzu ya Shirika la Umeme Tanzania ya ETDCO inayohusika na ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji ya umeme na kuwataka waongeze kasi ya ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wanayoitekeleza.

Ameiagiza kampuni hiyo kuwa, ikifikapo Mwezi wa 10 mwishoni nguzo zote za zege ambazo zinahitajika ziwe zimefika katika maeneo ya kazi (site) na kusimikwa na kwamba atafuatilia utekelezaji wake na kwa sababu kampuni hiyo imepewa fedha shilingi Bilioni 58 ili kuwaongezea ufanisi.


“Kwa ujumla tumekubaliana vifaa vya kazi vyote vinavyohitatija katika kazi hii, ikifika mwezi wa 12 viwe vimefika, na tutafika kuvikagua, pia tutakagua kazi inayotekelezwa na kazi kama haijafanyika kama tulivyokubaliana tutachukuwa hatua; kwa sababu kampuni hii ni ya ndani inatakiwa kufanya kazi kwa mfano mzuri ili iweze kuchagiza kampuni nyingine kufanya kazi kwa weledi na kwa ufanisi mkubwa sana, iwe jua iwe mvua ni lazima tukubaliane na tutekeleze yale tuliokubaliana bila kisingizo chochote, ikifika Mwezi Juni 2024 mradi huu uwe umekamilika na Katavi kuunganishwa katika Gridi ya Taifa,” amesisitiza Mhe. Kapinga.

/ Published posts: 1209

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram