135 views 45 secs 0 comments

MHANDISI SEFF AMTAKA MKANDARASI BARABARA YA KASULU-KABANGA-KASUMO-MUYAMA KUKAMILISHA MRADI KWA WAKATI

In KITAIFA
October 07, 2023

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mhandisi Victor H. Seff amemwelekeza Mkandarasi ‘Salum Motors Transport Co.Ltd’ kuhakikisha anakamilisha kwa wakati ujenzi wa barabara ya Kasulu- Kabanga-Kasumo-Muyama km 36 ambapo awamu ya kwanza ya km 12.5 inaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami.

Akiwa katika ukaguzi wa barabara hiyo, Mhandisi Seff ameeleza kuwa maagizo yaliyotolewa kwa Mkandarasi hapo awali yamefanyiwa kazi kwa kiasi kikubwa na kwamba hatarajii suala la maombi ya nyongeza ya muda.

“Leo nimekagua barabara hii kwa mkataba huu wa awamu ya kwanza km 12.5, kazi inaendelea na Mkandarasi anatakiwa kumaliza kazi hii ndani ya muda uliopangwa, kwa maana hiyo sitarajii kuona maombi ya nyongeza ya muda kwani hakuna sababu yoyote ya kufanya hivyo”, amesema Mhandisi Seff.

Kwa upande wake Bi. Naomi Kiogoma mkazi wa Kijiji cha Kasumo amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo ni mkombozi kwa wakazi wa vijiji hivyo kwani barabara ikikamilika wananchi wataweza kusafirisha mazao kwa urahisi kwenda Kasulu.

“Barabara hii itatusaidia hasa kukuza uchumi wetu, sisi akina mama sasa tutaweza kufanya biashara maana hata kama mtu anataka kuuza mazao kama maharage itakua rahisi kuyafikisha Kasulu”, amesema Bi. Naomi.

Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 36 inajengwa kwa awamu ya kwanza kilomita 12.5 kwa kiwango cha lami na inatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 18 ambapo itagharimu shilingi Bilioni 16.7

/ Published posts: 1209

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram