*Ujenzi wa daraja la Msangano lenye mita 56 watajwa
Wananchi wa Wilaya ya Momba Mkoani Songwe wameeleza kufurahishwa na ujio wa Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini TARURA Mhandisi Victor Seff aliyetembelea Vijiji mbalimbali vya Wilaya hiyo ndani ya Kata takribani sita na kujionea hali halisi ya ujenzi na matengenezo ya Barabara.
Mhandisi Seff akiambatana na Mbunge wa Jimbo la Momba Mhe. Condester Sichalwe amefika katika Kata ya Msangano na kujione eneo linapotarajiwa kujengwa Daraja la Msangano litakalokuwa na mita 56 ili kuunganisha Wilaya ya Momba na Tunduma.
Wakieleza furaha zao wananchi hao akiwemo Mwenyekiti wa Kijiji cha Mnyuzi Bwana Bonifansi Siwale ameeleza kuwa daraja hilo ni muhimu kwani kipindi cha masika wananchi wanapata shida sana kusafiri kutoka eneo hilo Kwenda Tunduma na Mbozi.
’’ Usafiri wa huku ni changamoto, Basi likishaondoka saa 11 asubuhi inakuwa ni vigumu kwa wananchi Kwenda Tunduma na Mbozi ambako ndo huduma muhimu zinapatikana’’. Amesema .
Naye, Mbunge wa Jimbo la Momba Mhe. Condester Sichalwe ameeleza kuwa daraja la Msangano ni muhimu kwa shughuli za kiuchumi na kijamiii hasa wakati wa masika kwani usafiri unakua washida kwa wananchi.
’’Kwa niaba ya wananchi wa jimbo la Momba natoa shukrani kwa serikali kupitia TARURA kwa kuamua kutenga fedha za ujenzi wa Daraja hili ili kurahisisha usafiri na usafirishaji kwa wananchi’’. Amesema Mhe Sichalwe.
Aidha, Mbunge huyo amempongeza Mtendaji Mkuu wa TARURA mhandisi Seff kwa kazi zinazoendelea kufanywa na Wakala kwa nchi nzima likiwemo jimbo la Momba na kwamba maeneo mengi sasa yanapitika na yale yenye changamoto jitihada za utatuzi zinaendelea ikiwa ni pamoja na mpango wa ujenzi wa Daraja la Msangano.
Akiongea na wananchi katika Kata hiyo ya Msangano Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Seff amewahakikishia kuwa tayari taratibu za manunuzi zimekamilika na mkandarasi wa ujenzi wa daraja hilo atafika ndani ya wiki mbili ili kuanza kazi ya ujenzi wa Daraja hilo unatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka mmoja.
’’ Niwahakikishie kwamba Serikali yenu sikivu tayari imetenga fedha za ujenzi wa daraja hili, mkandarasi amepatikana na ndani ya wiki mbili atakuwa hapa kuanza kazi hii ili huduma za usafiri na usafirishaji ziwe rahisi na hilo ndilo lengo la Serikali’’. Amesema Mhandisi Seff.
Vilevile ametoa wito kwa Vijana kuchangamkia fursa ya kufanya kazi katika eneo hilo kwa kipindi chote cha ujenzi wa daraja huku akiwaomba viongozi wa maeneo hayo kutoa ushirikiano kwa mkandarasi na kulinda vifaa vyote vya ujenzi ili kazi ikamilike kwa muda uliopangwa.