
Ufaransa imeamuru kusitishwa mara moja kwa mauzo ya simu zote za Apple aina iPhone 12 kutokana na kugundulika kuwa na mionzi mingi ya sumakuumeme (electromagnetic) ambayo si salama kiafya kwa watumiaji wake.
Shirika la uangalizi la Ufaransa (ANFR) liliiambia kampuni ya Apple kurekebisha simu zilizopo na kuipa ushauri kampuni hiyo, ikiwa haiwezi kutatua suala hilo basi iziondoe sokoni simu zote za iPhone 12.
Lakini Shirika la Afya Duniani hapo awali lilijaribu kuondoa hofu kuhusu mionzi hiyo kwa kusema hakuna ushahidi kuwa kiwango cha mionzi ya sumakuumeme ni hatari kwa binadamu.
IPhone 12 ilitolewa kwa mara ya kwanza mnamo Septemba 2020, na bado inauzwa Duniani kote.
Apple iliambia BBC News kuwa inapinga uhakiki wa ANFR, na ikasema imempa mdhibiti matokeo ya maabara kutoka kwa kampuni kubwa ya teknolojia yenyewe na wahusika wengine ambayo yanaonyesha kuwa kifaa hicho kinafuata sheria zote husika.
Ilisema iPhone 12 ilitambuliwa kama inatii kanuni za viwango vya mionzi duniani kote.