535 views 4 mins 0 comments

TIRDO NA REPOA KUANDAA KOZI YA UZALISHAJI MKAA MBADALA

In BIASHARA
September 12, 2023


TIRDO na REPOA imeandaa kozi ya mafunzo ya uzalishaji wa Mkaa Mbadala (Biomass Briquettes) ambayo ni nishati safi kwa matumizi ya majumbani, taasisi na hata viwandani.

Mafunzo hayo yanalenga kuimarisha umuhimu Kwa ustawi wa uchumi na mazingira na afya Kwa ujumla na uzalishaji Bora wa mkaa mbadala ambao unaotumia malighafi za taka za kilimo na misitu (agricultural and forest wastes)

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam Leo jumanne 12 September 2023 Mkurugenzi Mkuu – Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania -TIRDO Prof. Mkumbukwa Mtambo amesema mikakati, na njia bora (best practices) ya uzalishaji wa mkaa mbadala pamoja na upimaji ubora wa bidhaa inayozalishwa na aina ya nyenzo au mashine zinazotumika katika uzalishaji huo.

“tutaweza kujua ni kwa nini watumiaji wengi wa bidhaa unayozalisha wanabadili mawazo na kutumia nishati nyingine na sio mkaa mbadala. Ikiwa wewe ni mgeni kwenye uzalishaji huu au unatafuta kuongeza ujuzi ulionao, kozi hii inalenga kukuongezea ujuzi na ufahamu muhimu wa uzalishaji bora wa mkaa safi”Amesema Mtambo

Aidha Prof Mtambo amesema Mafunzo haya yametayarishwa baada ya kufanya utafiti katika mikoa 12 (asilimia 39) hapa nchini na kuweza kutembelea wazalishaji mkaa mbadala 58 na watumiaji 122. Utafiti huu ulifanywa na TIRDO kwa kushirikiana na REPOA ukiwa na lengo la โ€˜Kuimarisha Uzalishaji wa Mkaa Mbadala (Biomass Briquettes) na Kukuza Matumizi yake kwa Ajili ya Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi nchini Tanzania.

“Watafiti waliweza kuchukua sampuli 43 za mkaa mbadala kutoka kwa wazalishaji katika mikoa hiyo na kupima kwenye maabara ili kuangalia ubora wake. Matokeo ya upimaji huo ulipelekea TIRDO na REPOA kufanya uboreshaji mkaa huo baada ya kuwa na changamoto za viwango na ubora unaotakiwa kulingana na viwango vya nchi”. Aliongezea Prof Mtambo

Vile vile Mtambo amebainisha kuwa Baadhi ya matokeo ya upimaji huo yatakuwa ni moja ya maeneo ya mafunzo yatakayoanza leo ili kuweza kuonesha udhaifu katika ubora na jinsi ya kuboresha uzalishaji huo kulingana na viwango vya nchi. Juhudi hizi zimefanywa ili kuweza kukidhi lengo tajwa hapo juu na kuendana sambamba na Tamko la Mheshimiwa Rais (pamoja na Mwongozo wa nchi uliotayarishwa) la kuwa na nishati safi ya kupikia mpaka ifikapo mwaka 2030.

“Wakati tunafanya maboresho ya uzalishaji wa mkaa huo, ilibidi kusanifu baadhi ya mashine ili kuweza kupata ubora unaotakiwa. Watafiti wameweza kusanifu mashine ya kuchomea malighafi za bayomasi (eco-carbonizer) yenye uwezo wa kupunguza nishati ya kuchomea kwa asilimia hamsini (50%), kuvuna joto ambalo linatumika kukaushia mkaa na pia kuvuna vinega. Vilevile, watafiti waliweza kuandaa Mwogozo ambao utatumika kwenye mafunzo, na ninaamini utaimarisha sana safari yenu ya kuongeza ujuzi wa uzalishaji bora wa nishati ya mkaa mbadala”. Aliongezea Prof Mtambo

Hata hivyo prof Mtambo amesema Kutokana na ufinyu wa fedha, watafiti hawakuweza kufika mikoa yote ya Tanzania, na ni asilimia 39 tu imeweza kufikiwa. Vilevile, watafiti hawakuweza kuwatembelea wazalishaji wote katika mikoa hiyo. Kwa muktadha huu, TIRDO kwa kushirikiana na REPOA inaangalia uwezekano wa kupata fedha ya kuweza kukamilisha takribani asilimia 61 ya mikoa iliyobakia. Sambamba na hilo mafunzo haya yatawafikia wazalishaji ishirini na mbili (22) tu kati ya hamsini na nane (58) waliofikiwa kutokana na ufinyu wa bajeti. Hata hivyo, kuna uhitaji mkubwa sana wa mafunzo haya kwa wajasiriamali, kwani wadau ambao hawajaalikwa wameonyesha kusikitika na wanakiu yakupata elimu hii.


Katika kozi hii, kutakuwa na mazingira mazuri ya kusaidiana na kushirikiana ili kurahisisha uelewa mzuri wa kila mshiriki wa mafunzo yatakayotolewa. Mafunzo hayo yatakuwa ya nadharia na vitendo ili kumwezesha kila mshiriki kupata ujuzi unaotakiwa na kwenda kuutumia katika eneo lake la kazi.

MADINA MOHAMMED

/ Published posts: 1486

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram