312 views 3 mins 0 comments

RUWASA KUNUFAISHA VIJIJI 11 MRADI WA MAJI NACHINGWEA

In KITAIFA
August 24, 2023

Jumla ya Vijiji vipatavyo 11 kutoka Kata 4 Naipanga, Chiumbati,
Rahaleo na Stesheni Wilayani Nachingwea Mkoani Lindi vinatarajia kunufaika na mradi wa huduma ya maji safi na salama wa Naipanga wenye jumla ya thamani ya sh.bil.1,187,057,785

Hayo yalibainishwa jana na Meneja wa Wakala wa Maji na usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA ) Wilayani hapo na Mhandisi Sultan Ndoliwa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuutambulisha mradi huo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea Mohamed Moyo, na wajumbe wa Halmashauri kuu ya Vijiji hivyo.

Mhandisi Ndoliwa amesema mradi wa Maji wa Naipanga upo katika kata ya Naipanga, Chiumbati, Rahaleo na Stesheni

” Mradi huu unajengwa chini ya Mpango wa lipa kwa matokeo ( Payment for Result-PforR ) na kusimamiwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini ( RUWASA )” amesema Mhandisi Ndoliwa.

Aidha amesema Mradi wa Maji wa Naipanga utatekelezwa na Mkandarasi Broadway Engineering Co Ltd- Dar Es Salaam kwa gharama ya sh.bilioni.1,187,057,785 na VAT kwa muda wa miezi 12 na Utekelezaji wake unaanza rasmi Leo Agost 22, Mwaka huu na kukamilika Agost 22, 2024.

Mhandisi Ndoliwa ameongeza kuwa mradi unatarajia kutoa huduma kwenye Vijiji 11 vya Chiumbati shuleni, Chiwindi, Tandika, Luagala, Rahaleo, Maendeleo, Kilombelo, Naipanga, Nagaga, Joshoni na Chekeleni ambapo utahudumia watu wapatao 19,110 kwa kuzingatia ratiba ya mgawanyo wa Maji ya WANAWASA.

” Mradi una tenki la ujazo wa Lita 300,000 na uzio, vituo vya kuchotea maji vyenye sehemu 2 kila kimoja na Mtandao wa mabombawenye urefu wa kilometa 32,425 ” amesema Mhandisi Ndoliwa.

Aidha alifafanua kuwa kazi zote za mradi zilizopangwa kufanyika zimekamilika ambazo ni Ujenzi wa tenki la maji la ujazo wa Lita 300,000, Ujenzi wa Vioksi 35, Ujenzi wa Vilula ( DPs ) na Uchimbaji mitaro na ulazaji Bomba kilometa 32,425.

Hata hivyo RUWASA inawaomba wanufaika wa mradi huo kuhakikisha inampa ushirikiano Mkubwa Mkandarasi husika ili aweze kufanikisha majukumu yake Kwa wakati uliokusudiwa.

Kwa upande wa wananchi Joyce Silvester Karembo amempongeza Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan Kwa kuwakumbuka na kupeleka mradi wa Maji katika Kijiji Cha Rahaleo jambo ambalo wanamshukuru sana ambapo awali walikua wakiishi katika Mazingira magumu sana juu ya upatikanaji wa Maji.

” Hakika maji ndio kila kitu katika maisha yetu, na hakuna chochote kitafanyika katika shughuli zetu za nyumbani bila ya maji, mama umetuheshimisha sana kutuletea mradi wa Maji nasema tumeupokea mrdi huu Kwa mikono miwili, Kwa nderemo na vifijo, tuliteseka sana lakini Leo Mungu ametuoana Asante sana Rais wetu, mama yetu Dkt.Samia Suluhu Hassan” amesema Joyce Karembo

Hata hivyo Mzee Mfalme Daudi Nyundo naye amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapeleka maji kwani ataweza hata kuoga mara mbili kwa siku, ambapo amedai kuwa zile ndoto walizokua wakiota ota hatimaye sasa zimekua kweli na hivyo kumtakia Rais Dkt.Samia maisha marefu, afya njema katika utendaji wake wa kazi.

Meneja wa wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini RUWASA Muhandisi Sultan Ndoliwa akizungumza na waandishi wa habari
/ Published posts: 1214

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram