313 views 2 mins 0 comments

BASATA KUWATANGAZA MABALOZI WAPYA NA KUFUFUA SEKTA YA SANAA

In BURUDANI
August 15, 2023

BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA) limewatambulisha rasmi Mabalozi watakaoshirikiana ili kupanua wigo wa mawazo na kutangaza Falsafa yake iliyojikita katika Kufufua Zaidi, Kukuza Zaidi na Kuendeleza zaidi Sekta ya Sanaa na kuipa mawanda mapana ya ubunifu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 15 Jijini Dar es Salaam akitambulisha mabalozi hao Katibu Mtendaji wa BASATA Dkt. Kedmon Mapana amesema kwa mujibu wa mtiririko wa utekelezaji wa shughuli za Sanaa nchini Baraza limedhamiria kuwa na Mabalozi watakaofanya kazi ya kulitangaza na kuwa wawakilishi wa Baraza katika kutekeleza majukumu yake ndani na nje ya nchi ili kuitambulisha kuwa ni Taasisi inayoshughulikia mustakabali wa maendeleo ya Wasanii na wadau wa Sanaa nchini.

Kwamba katika kufanikisha hilo Dkt. Mapana amesema Baraza limefanya maamuzi ya kuwachagua Ritha Paulsen (Madam Ritha) na Mrisho Mpoto (Mjomba) kuwa Mabalozi watakaofanya kazi kuhakikisha wanalitangaza Baraza kwa wadau wao ili wafahamu Falsafa ya Utekelezaji wa Shughuli zao.

โ€œUshirikiano huu wa Baraza na mabalozi umejikita katika makubaliano ya kufanya kazi kwa muda wa Miezi 12 kuanzia leo ambapo tutasaini mkataba wa maridhiano,โ€ ameeleza Dkt. Mapana.

Dkt. Mapana ameongeza kwamba mabalozi hao wamelihakikishia Baraza kuwa wanao uwezo wa kuifanya kazi hiyo kwa kupitia ushawishi na uzoefu walio nao kwenye tasnia ya sanaa hivyo wadau wao wakae tayari kwa mambo mazuri yajayo.

Ametaja maeneo ya msingi ambayo watashughulika nayo kwenye kulitangaza Baraza kuwa ni pamoja na kutumia vyombo vya habari au mitandao ya kijamii kutangaza shughuli za Baraza pamoja na kushiriki katika warsha au matukio mbalimbali ya Sanaa ambapo watatumia majukwaa hayo kuwafikia wadau na kulitangaza Baraza.

Katibu Mtendaji huyo amebainisha kuwa Baraza limedhamiria kuwafikia wadau wake kwa wakati ndiyo maana limeamua kutumia mfumo huu wa kuwa na mabalozi hao.

Amesema ni matarajio yao kuwa watapata ushirikiano wa kutosha wenye lengo la kuiendeleza Sekta ya Sanaa nchini.

/ Published posts: 1883

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram