
Mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai Tanzania (DCI) Kamishna wa Polisi Ramadhani Kingai ambaye pia ni msimamizi na mfuatiliaji wa Kanda namba mbili ya mashariki iliyojumuisha Kanda Maalum Dar es salaam, Pwani na Rufiji.

Kamishna Kingai amewataka Askari wa Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua wanunuzi wa mali za wizi “Receivers” kwa vile wao pia ni wahalifu.
Hayo ameyasema wakati alipofanya kikao kazi na Maafisa, Wakaguzi na Askari wa vyeo mbalimbali wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam. Kikao kazi hicho kimefanyika katika ukumbi wa mikutano wa bwalo la Polisi Kilwa road leo Agosti 8, 2023.
Aidha amewasisitiza askari kuzidisha bidii ya kuwaelimisha wananchi ili watambue kwamba upelelezi unatakiwa ufanyike kabla ya kukamatwa mtuhumiwa ili mtuhumiwa anapokamatwa, yaandaliwe mashtaka na kupelekwa mahakamani kwa baadhi ya makosa na ikiwa kama kosa alilofanya linadhaminika mtuhumiwa anaweza kuachiwa huru kwa misingi ya kisheria wakati upelelezi ukiwa unaendelea.

Katika hatua nyingine amewataka wananchi kuaacha tabia ya kushindikiza kutaka kukamatiwa mtuhumiwa na kuwekwa kwenye mahabusu za Polisi kinyume na utaratibu na miongozo ya kisheria.
Pia amesisitiza kutumia viongozi wa kidini kupitia falsa ya Polisi jamii ili kusaidia jamii kujiepusha na vitendo vya kihalifu kwa vile watakuwa wamejengwa kiroho na kuendelea kufanya mambo mema yanayopendaza kwa Mungu na kwa jamii.
Kamishna Kingai amesifu na kuwapongeza askari wa Dar es Salaam kwa kazi nzuri wanazoendelea kuzifanya na kuhakikisha vitendo vya kihalifu vimedhibitiwa na jamii kuendelea na harakati zao za kila siku.
Amehitimisha kikao hicho kwa kuwasisitiza kila mmoja kutekeleza wajibu wake pasi na mivutano kwa kuzingatia nidhamu, haki weledi na uadilifu.