143 views 5 mins 0 comments

MTANZANIA ATEKWA NCHINI NIGERIA

In KITAIFA
August 07, 2023

Mtanzania ambaye ni frateri wa Shirika la Wamisionari wa Afrika (White Fathers) mzaliwa wa Parokia ya Kabanga, Jimbo la Kigoma, Melkiori Mahinini (27) ametekwa nyara na watu wasiojulikana nchini Nigeria.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Kigomba, Joseph Mlola, mseminari huyo alikamatwa Agosti 4 mwaka huu katika jimbo la Minna huko Nigeria akiwa na mwenzake, Padri Paul Sanogo, raia wa Burkina Faso.

“Walitekwa na kundi la watu wasiojulikana mapema usiku wa kuamkia Agosti 3, 2023 katika Parokia ya Mtakatifu Luka Gyedna, jimbo la Minna nchini Nigeria. Mseminari wetu huyu alikuwa katika mwaka wake wa uchungaji kabla ya kuanza masomo ya teolojia.

“Tumwombe Mungu asikilize sala zetu na awanusuru katika hatari zozote na awarudishe katika amani, mwanga na uhuru kamili,” alisema Askofu Mlola katika taarifa yake kwa waumini na Taifa kwa ujumla.

Kufuatia ya taarifa hiyo ambayo imesambaa pia mitandaoni, gazeti hili lilimtafuta Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Dk Benson Bana ambaye alikiri kuwepo kwa tukio hilo na kwamba wanachukua hatua mbalimbali kuhakikisha Mtanzania huyo pamoja na mwenzake wa Burkina Faso wanaachiwa huru.

Balozi Bana alisema matukio ya watu kutekwa nchini Nigeria yamekuwa mambo ya kawaida na kwamba wanachukua tahadhari kubwa ili watekaji hao wasiwadhuru mateka, bali waachiwe huru wakiwa wazima.

“Tulipopata taarifa hizi tulichukua hatua mbili; kwanza, tulitoa taarifa kwa Serikali huko nyumbani (Tanzania), pili, tuliwapa taarifa wenzetu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria kama taratibu za kidiplomasia zinavyotaka,” alisema Balozi Bana.

Balozi huyo alisema siku ya tukio, kikundi cha watu wasiojulikana kilivamia Parokia ya Mtakatifu Luka Gyedna huku kikipiga risasi nyingi hewani na kufanikiwa kuwateka nyara watu wawili kati ya wanne waliokuwepo.

Alisema taarifa alizozipata ni kwamba watekaji wanataka Naira 100 milioni (sawa na Sh325.1 milioni) ili kuwaachia huru wote wawili. Alisema wamepiga hesabu na kuona kwamba kila mmoja anatakiwa kulipiwa karibu Dola 70,000 za Marekani 70,000 (zaidi ya Sh170 milioni).

“Tunahitaji kuwa waangalifu katika jambo hili kwa sababu watu hawa si wazuri, wakijua kwamba Serikali italipa wataongeza dau hadi Naira 500 milioni. Kwa hiyo, tunaendelea kushirikiana na wenzetu wa Shirika la Wamissionari wa Afrika ambao tayari wametoa taarifa polisi,” alisema.

Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga ameeleza kusikitishwa na tukio hilo akisema “tunasikitishwa sana na kitendo hicho cha kikatili cha kuwateka nyara binadamu. Tunasisitiza umuhinu wa kuheshimu haki msingi na utu wa binadamu.”

Alisema, “tunachochea jitihada za kidiplomasia za kuhakikisha watu waliotekwa wanaachwa huru bila masharti. Tunasali kumwomba Mungu awaokoe ndugu zetu.”

Baba mzazi wa mseminari huyo, Dominiki Mahinini akizungumza na gazeti hili ameiomba Serikali kwa kushirikiana na Kanisa Katoliki kumsaidia ili mtoto wake aweze kupatikana.

Baba huyo mkazi wa mtaa wa Masanza, kata ya Kabanga, wilayani Kasulu, alisema taarifa hizo za kutekwa kwa mtoto wake alizipata Alhamisi ya Agosti 3, kutoka kwa Paroko na kwamba hadi sasa hajui yuko wapi.

“Serikali ina mkono mrefu, inaweza kufika popote na kuhakikisha kijana wangu anapatikana, naiomba inisaidie mimi sina uwezo wa kufanya chochote kwa sasa zaidi ya kumuomba Mungu,” alisema Mahinini.

Alisema analiomba Kanisa Jimbo Katoliki Kigoma liweze kushirikiana na Serikali ya Tanzania ili kijana wake aweze kupatikana na kama wakijua alipo hao waliomshikilia waseme wanahitaji nini ili waweze kumuachia kijana wake.

Alisema wao kama familia hadi sasa hawana cha kufanya kwani taarifa hizo wamezipokea kwa mshtuko ulioleta taharuki na hawajui hatua gani wazichukue.

Mahinini alisema Melkiori mtoto wa watano kati ya watoto wake tisa, alikuwa na wito wa kumtumikia Mungu tangu akiwa mdogo, hali iliyomfanya yeye kama mzazi kumsadia kutimiza ndoto zake ikiwemo kumpeleka kupata elimu katika shule za seminari.

“Katika familia yangu yeye ndiye mtoto pekee a anayemtumikia Mungu, wengine wote bado wanasoma. Na hata kama wakitokea hapo baadaye na kutaka kujitoa maisha yao kwa utumishi sitawazuia nitawasaidia kutimiza ndoto zao,” alisema.

Mdogo wake Melkiori, Libratus Mahinini (22), alisema kaka yake baada ya kumaliza kidato cha sita alichukuliwa na shirika la White Fathers kuendeleza hitaji lake la kumtumikia Mungu.

/ Published posts: 1214

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram