
LEO Jumapili linafanyika Tamasha la Simba Day kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar, ambapo kutakuwa na burudani mbalimbali, kisha kikosi cha Simba SC kwa msimu wa 2023/24 kitatambulishwa rasmi, ikifuatiwa na mechi ya kirafiki kati ya Simba dhidi ya Power Dynamos.
Kuelekea tamasha hilo, Wanasimba wameendelea kuwatambia wapinzani wao wakiwaambia: “Njooni muige, Simba raha tupu, sisi ndiyo wakali wa hizi kazi.”
Tamasha hilo likiwa linafanyika leo Agosti 6, lakini tayari tiketi za kuingia uwanjani zimemalizika zote tangu Agosti 3, mwaka huu, hiyo ni rekodi imewekwa, kitu ambacho Simba wanajivunia nacho.
Mgeni rasmi katika tamasha hilo leo, anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Kuelekea shughuli hiyo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema: “Mageti yatafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi. Tunawasisitiza wale wote ambao hawajanunua tiketi, kesho (leo) wasisogee eneo la Uwanja wa Benjamin Mkapa. Kama huna tiketi kaa nyumbani, Jeshi la Polisi Iinasisitiza ili kupunguza usumbufu usio wa lazima.”
Hili ni tamasha la 15 kufanyika tangu kuanzishwa kwa Simba Day 2009, katika mechi 14 za kirafiki zilizochezwa kunako matamasha 14 yaliyopita, Simba imeshinda nane, imepoteza nne na sare mbili. Huku ikifunga mabao 24 na kuruhusu 11.