270 views 4 mins 0 comments

RUWASA YAJIPANGA VYEMA UTOAJI HUDUMA YA MAJI VIJIJINI

In KITAIFA
August 05, 2023

Meneja Uhusiano na masoko wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Athumani Shariff amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa RUWASA mwaka 2019 wamekuwa kila mwaka wakishiriki maonesho ya kilimo kwa maana ya Nane Nane katika Mikoa ya Simiyu na Mbeya kutokana na mamlaka hiyo kuwa mdau mkubwa wa sekta ya kilimo nchini.

Meneja huyo amesema kuwa kila mwaka lazima washiriki nane nane kwa sababu ni wadau wa sekta ndogo ya maji vijijini kwa maana RUWASA wanajenga, wanaosanifu miradi na kuhakikisha kuwa wananchi wanaoishi vijijini wanapata huduma ya maji safi na salama na ya kutosheleza.

Shariff amesema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa Habari kwenye banda la Mamlaka hiyo kwenye sherehe za maonesho ya kimataifa ya kilimo Nane nane yanayoendelea katika viwanja vya John Mwakangale katika Jiji la Mbeya.

“Lakini kama mnavyofahamu pasipo maji hakuna uhai iwe ni kwa mifugo, kwa binadamu hata kwa mimea na tumekuwa tukishiriki maonesho ya Nane nane kwa sababu yanakutanisha wadau wengi sana wa vijijini ukilinganisha na maonesho ya Sabasaba hivyo tumeona ni fursa nzuri ya kukutana na wadau wetu wa vijijini kuwaelimisha kuhusu RUWASA,” amesema Athumani Shariff Meneja Uhusiano na Masoko RUWASA.



Aliendelea kusema kuwa RUWASA ni wadau wakubwa na wananchi wengi wanaishi vijijini na RUWASA ndiyo inayotoa huduma ya maji vijijini na kuongeza kuwa ili mfugaji aweze kufuga vizuri siyo tu anahitaji malisho ni lazima apate maji safi na salama kwake yeye mwenyewe mfugaji lakini hata kwa mifugo yake.

Kutokana na hali hiyo RUWASA inashiriki kuwajengea mabwawa ya maji, pia wanashiriki kuwajengea wafugaji malambo kwa ajili ya kunyweshea mifugo lakini pia wanahakikisha wanapata huduma safi ya maji mazuri ambayo hata wanyama wao wakiyatumia hawatapata madhara kwa sababu maji ya RUWASA ni ya uhakika yamepimwa yana vigezo vyote vya kutumika kwa maana ya binadamu, wanyama na hata kwa kilimo.

“Kilimo nacho kinahitaji maji iwe bustani ndogondogo lakini hata kwa mashamba makubwa, sisi kama RUWASA tunahakikisha pia tunashirikiana na sekta ya kilimo kuhakikisha pia wanapata maji safi na salama kwaajili ya kutosheleza,” alisema Shariff.

Ameongeza kuwa tayari Rais Samia Suluhu Hassan ametoa vifaa vya kuchimbia mabwawa mitambo 5 ipo kila Kanda, lakini pia amewapa mitambo 25 ya kuchimbia visima katika mikoa yote ya Tanzania bara na kila mkoa mmoja una mtambo isipokuwa mkoa wa Dar es Salaam na kwamba mitambo hiyo inachimba visima siyo tu kwaajili ya binadamu bali maji hayo yananufaisha mifugo, wanyama na hata wakulima ambao wanahitaji kuchimbiwa visima kwaajili ya skimu zao za kilimo cha umwagiliaji.

Amesema kuwa RUWASA ni wadau wakubwa wa kilimo pia na sekta ya mifugo na uvuvi na kufafanua kuwa wafugaji wa samaki wanahitaji mabwawa, wanahitaji maji hivyo RUWASA ndiyo wanajukumu la sekta ndogo ya maji vijijini.

Pamoja na mambo mengine amesema kuwa mamlaka hiyo imekuwa mdau muhimu wa maonesho ya nane nane jijini Mbeya na wapo karibu sana na sekta ya kilimo na mifugo.

Amesema kuwa mpaka sasa wapo asilimia 77 ya huduma ya maji vijijini na lengo ifikapo mwaka 2025 wawe wamefika zaidi ya asilimia 85 kwa upande wa vijijini na kufafanua kuwa wenzao wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira mijini wanatakiwa wawe wamefika zaidi ya asilimia 95. Na ifikapo mwaka 2030 wanatakiwa wawe wamefika asilimia 100 ya huduma ya maji vijijini kazi inayokuwa imebaki ni kuhakikisha kuwa huduma ya maji iwe endelevu.

Kauri mbiu “Vijana na wanawake ni msingi imara wa mifumo endelevu na chakula”.

Madina Mohammed

/ Published posts: 1214

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram