157 views 3 mins 0 comments

TPDC IPO KATIKA MIPANGO YA UKARABATI WA VISIMA VYA UZALISHAJI GESI

In KITAIFA
July 28, 2023

SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeeleza juhudi zinazofanywa katika kuhakikisha nishati ya Gesi inapatikana kwa uhakika na hatimaye kuwezesha upatikanaji wa nishati ya uhakika ya umeme nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 28, 2023 jijini Dar es Salaam Kaimu Meneja Uendelezaji wa Uzalishaji wa Gesi TPDC Mhandisi Felix Nanguka amesema kwamba ipo katika mipango ya kuanza utekelezaji wa zoezi la ukarabati wa visima vya uzalishaji Gesi ambalo litafanyika katika Kitalu cha Mnazi Bay kilichopo Mtwara kwa kushirikiana na Mkandarasi wa Kitalu hicho.

“Zoezi hili ni laukarabati wa visima kwa ajili ya mwendelezo wa gesi ambayo inazalishwa hapa nchini, kuhakikisha hivi visima vinakuwa na gesi katika ufanisi ule ule,” amesema Mhandisi Nanguka.

Kwamba pamoja na zoezi hilo wanatarajia kuongeza uzalishaji katika kisima namba moja ambacho kinatoa Gesi kwa ajili ya umeme ambao unazalishwa mkoani Mtwara kwa matumizi ya mikoa ya Mtwara na Lindi.

Mhandisi Nanguka amesema Kisima hicho pia kinachangia kwenye Gesi inayoingia kwenye Bomba kubwa linalotela Gesi mkoani Dar es Salaam kwa ajili ya matumizi ya Gridi ya Taifa na Matumizi mengine ya Viwandani.

“Kwasasa hiki kisima kina uwezo wa kuzalisha takribani futi za ujazo milioni 11 kwa siku na tunatarajia baada ya zoezi hili kiasi cha futi za ujazo bilioni saba zitaongezeka. Hivyo kuongeza ufanisi wa kisima hiki kwa asilimia 65 ,” ameeleza Mhandisi Namguka na kuongeza,

“Kwa sasa kama mnavyojua uzalishaji wa umeme hapa nchini unatokana na zaidi ya asilimia 65 ya Gesi inayozalishwa hapa nchini. Na pia ikumbukwe kwamba kati ya kiasi chote ambacho TPDC na washirika wake wanazalisha hapa nchini basi asilimia 84 hadi 85 inaenda moja kwa moja kwenye matumizi ya umeme,”.

Hivyo amesema kwamba zoezi hilo wanalofanya ni muhimu zaidi kwa sababu litasaidia kuongeza kiwango cha umeme ambapo amebainisha kuwa futi za ujazo bilioni saba zitakazoongezeka zitaongeza takribani megawati 35 za umeme.

Aidha amesema TPDC pia ina mipango ya kuongeza uzalishaji kwenye visima vingine vinavyozalisha gesi nchini ikiwemo katika Kitalu cha Songosongo kilichopo Kilwa Kisiwani ambapo amesema huko kuna zoezi la ufungaji wa kompresa kubwa itakayoongeza uzalishaji wa Gesi.

“Mipango inaendelea, pia ukarabati wa visima utafanyika kule, hivyo tunajua tutaongeza kiasi cha gesi,” amesema Mhandisi Nanguka.

Kadhalika amesema kuna kitalu kipya kilichopo mkoani Mtwara ambacho kinaitwa Mtoria ambacho wanatarajia kukifanyia uendelezwaji mpya ambapo mategemeo ni gesi kuanza kuzalishwa mwaka 2025.

Amesema kwa kitalu hicho pia wataanzia na futi za ujazo milioni 60 kwa siku na utaongezeka hadi kufikia futi za ujazo milioni 140 kwa siku.

Kwamba pamoja na juhudi hizo, pia katika kitalu cha Mnazi Bay kwa baadaye wanatarajia kuongeza uzalishaji kwenye baadhi ya visima ambavyo wataboresha kwa kutoboa njia mpya za uzalishaji pamoja na kuangalia uwezekano wa kuchimba visima vipya.

Madina Mohammed

/ Published posts: 1215

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram